Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waebrania 9:1-15

Waebrania 9:1-15 NENO

Basi agano lile la kwanza lilikuwa na kanuni zake za kuabudu na pia patakatifu pake pa kidunia. Hema ilitengenezwa. Katika sehemu yake ya kwanza kulikuwa na kinara cha taa, meza na mikate iliyowekwa wakfu; hii sehemu iliitwa Mahali Patakatifu. Nyuma ya pazia la pili, palikuwa na sehemu iliyoitwa Patakatifu pa Patakatifu, ambapo palikuwa na yale madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba, na lile Sanduku la Agano lililofunikwa kwa dhahabu. Sanduku hili lilikuwa na gudulia la dhahabu lenye mana, ile fimbo ya Haruni iliyochipuka, na vile vibao vya mawe vya Agano. Juu ya lile Sanduku kulikuwa na makerubi wa Utukufu, wakikitia kivuli kiti cha rehema. Lakini hatuwezi kujadili vitu hivi kwa undani sasa. Basi vitu hivi vilipokuwa vimepangwa, makuhani waliingia mara kwa mara katika sehemu ya kwanza ya hema ili kufanya taratibu zao za ibada. Lakini ni kuhani mkuu peke yake aliyeingia ndani ya sehemu ya pili ya hema. Tena hii ilikuwa mara moja tu kwa mwaka, na hakuingia kamwe bila damu, ambayo alitoa kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi za watu walizotenda bila kukusudia. Kwa njia hii, Roho Mtakatifu alikuwa anaonesha kwamba, maadamu lile hema la kwanza lilikuwa bado limesimama, njia ya kuingia Patakatifu pa Patakatifu ilikuwa bado haijafunguliwa. Huu ulikuwa mfano kwa ajili ya wakati wa sasa, kuonesha kwamba sadaka na dhabihu zilizokuwa zikitolewa hazikuweza kusafisha dhamiri ya mtu anayeabudu. Lakini hizi zilishughulika tu na vyakula na vinywaji, pamoja na taratibu mbalimbali za kunawa kwa nje, kanuni kwa ajili ya mwili zilizowekwa hadi wakati utimie wa matengenezo mapya. Kristo alipokuja akiwa Kuhani Mkuu wa mambo mema ambayo tayari yameshawasili, alipitia kwenye hema iliyo kuu zaidi na bora zaidi, ambayo haikutengenezwa kwa mikono ya binadamu, hii ni kusema, ambayo si sehemu ya uumbaji huu. Hakuingia kupitia kwa damu ya mbuzi na ya ndama; lakini aliingia Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kwa damu yake mwenyewe, akiisha kupata ukombozi wa milele. Damu ya mbuzi na ya mafahali, na majivu ya mitamba walivyonyunyiziwa wale waliokuwa najisi viliwatakasa, hata kuwaondolea uchafu wa nje. Basi damu ya Kristo, ambaye kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na waa, si itazisafisha dhamiri zetu zaidi kutokana na matendo yaletayo mauti, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai! Kwa sababu hii Kristo ni mpatanishi wa agano jipya, ili wale walioitwa waweze kupokea ile ahadi ya urithi wa milele: kwa vile yeye alikufa awe ukombozi wao kutoka kwa dhambi walizozitenda chini ya agano la kwanza.