Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waebrania 11:21-40

Waebrania 11:21-40 NENO

Kwa imani Yakobo alipokuwa anakufa, alimbariki kila mmoja wa mtoto wa Yusufu, akamwabudu Mungu akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake. Kwa imani, Yusufu alipokaribia mwisho wa maisha yake, alinena habari za kutoka kwa Waisraeli huko Misri na akatoa maagizo kuhusu mifupa yake. Kwa imani, wazazi wa Musa walimficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa, kwa sababu waliona kuwa si mtoto wa kawaida, wala hawakuiogopa amri ya mfalme. Kwa imani, Musa alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu, kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa muda mfupi. Aliona kushutumiwa kwa ajili ya Kristo ni utajiri mkubwa kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye. Kwa imani Musa aliondoka Misri bila kuogopa ghadhabu ya mfalme. Alivumilia kwa sababu alimwona yeye asiyeonekana kwa macho. Kwa imani akaadhimisha Pasaka na kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wazaliwa wa Israeli. Kwa imani, watu walivuka Bahari ya Shamu kama vile juu ya nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo, walitoswa ndani ya maji. Kwa imani kuta za Yeriko zilianguka, baada ya watu kuzizunguka kwa siku saba. Kwa imani, Rahabu, yule kahaba, hakuangamizwa pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi. Basi niseme nini zaidi? Sina wakati wa kusema habari za Gideoni, Baraka, Samsoni, Yefta, Daudi, Samweli na manabii, ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitekeleza haki, na wakapokea ahadi za Mungu; walifunga vinywa vya simba, wakazima makali ya miali ya moto, na wakaepuka kuuawa kwa upanga; udhaifu wao uligeuka kuwa nguvu; pia walikuwa hodari vitani na kuyafukuza majeshi ya wageni. Wanawake walipokea watu wao waliokuwa wamekufa, wakafufuliwa. Lakini wengine waliteswa, nao wakakataa kufunguliwa, ili wapate ufufuo ulio bora zaidi. Wengine walidhihakiwa na kupigwa, hata walifungwa minyororo na kutiwa gerezani. Walipigwa kwa mawe; walipasuliwa vipande viwili kwa msumeno; waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na mbuzi, wakiwa maskini, wakiteswa na kutendwa mabaya, watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao. Walizunguka majangwani na milimani, katika mapango na katika mahandaki ardhini. Hawa wote walishuhudiwa vyema kwa sababu ya imani yao, lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea yale yaliyoahidiwa. Kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea kitu kilicho bora zaidi ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.