Mwanzo 50:14-26
Mwanzo 50:14-26 NENO
Baada ya Yusufu kumzika baba yake, akarudi Misri pamoja na ndugu zake na wale wote waliokuwa wameenda naye kumzika baba yake. Ndugu zake Yusufu walipoona kwamba baba yao amekufa, wakasema, “Itakuwaje kama Yusufu ataweka kinyongo dhidi yetu na kutulipa mabaya yote tuliyomtendea?” Kwa hiyo wakampelekea Yusufu ujumbe, wakasema, “Kabla baba yako hajafa aliacha maagizo haya: ‘Hili ndilo mtakalomwambia Yusufu: Ninakuomba uwasamehe ndugu zako dhambi na mabaya kwa vile walivyokutenda vibaya.’ Sasa tafadhali samehe dhambi za watumishi wa Mungu wa baba yako.” Ujumbe huu ulipomfikia, Yusufu akalia. Ndipo ndugu zake wakaja na kujitupa chini mbele yake. Wakasema, “Sisi ni watumwa wako.” Lakini Yusufu akawaambia, “Msiogope. Je, mimi ni badala ya Mungu? Mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, ili litimie hili linalofanyika sasa, kuokoa maisha ya watu wengi. Hivyo basi, msiogope. Mimi nitawatunza ninyi nyote pamoja na watoto wenu.” Akawafariji na kusema nao kwa wema. Yusufu akakaa katika nchi ya Misri, yeye pamoja na jamaa yote ya baba yake. Akaishi miaka mia moja na kumi, naye akaona kizazi cha tatu cha watoto wa Efraimu. Pia akaona watoto wa Makiri mwana wa Manase, wakawekwa magotini mwa Yusufu walipozaliwa. Ndipo Yusufu akawaambia ndugu zake, “Mimi ninakaribia kufa. Lakini kwa hakika Mungu atawasaidia na kuwachukueni kutoka nchi hii na kuwapeleka katika nchi aliyomwahidi kwa kiapo Abrahamu, Isaka na Yakobo.” Naye Yusufu akawaapisha wana wa Israeli na kuwaambia, “Hakika Mungu atawasaidia, nanyi ni lazima mhakikishe mmepandisha mifupa yangu kutoka mahali hapa.” Kwa hiyo Yusufu akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi. Baada ya kumtia dawa asioze, akawekwa kwenye jeneza huko Misri.