Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 46:26-34

Mwanzo 46:26-34 NENO

Wote walioenda Misri pamoja na Yakobo, waliokuwa wazao wake hasa pasipo kuhesabu wakwe wake, walikuwa watu sitini na sita. Pamoja na wana wawili waliozaliwa na Yusufu huko Misri, jumla ya jamaa ya Yakobo walioenda Misri walikuwa sabini. Basi Yakobo akamtanguliza Yuda aende kwa Yusufu ili amwelekeze njia ya Gosheni. Walipofika nchi ya Gosheni, Yusufu aliandaa gari lake la vita, na akaenda Gosheni kumlaki baba yake, Israeli. Mara Yusufu alipofika mbele yake, alimkumbatia baba yake, akalia kwa muda mrefu. Israeli akamwambia Yusufu, “Sasa niko tayari kufa, kwa kuwa nimejionea mwenyewe kwamba bado uko hai.” Ndipo Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, “Nitapanda kwa Farao na kumwambia, ‘Ndugu zangu na watu wa nyumbani mwa baba yangu, walioishi katika nchi ya Kanaani, wamekuja kwangu. Watu hao ni wafugaji; wao huchunga mifugo, na wamekuja na makundi ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, pamoja na kila kitu walicho nacho.’ Farao atakapowaita na kuwauliza, ‘Kazi yenu ni nini?’ mjibuni, ‘Watumishi wako wamekuwa wafugaji wa wanyama tangu ujana wetu hadi sasa, kama baba zetu walivyokuwa.’ Ndipo mtaruhusiwa kukaa katika nchi ya Gosheni, kwa kuwa wafugaji wote ni chukizo kwa Wamisri.”