Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 43:15-28

Mwanzo 43:15-28 NENO

Basi hao watu wakazichukua zile zawadi na zile fedha mara mbili pamoja na Benyamini. Wakafanya haraka kwenda Misri na wakajionesha kwa Yusufu. Yusufu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Wachukue watu hawa nyumbani mwangu, mchinje mnyama na kuandalia chakula, kwa kuwa watakula chakula cha mchana pamoja nami.” Msimamizi akafanya kama Yusufu alivyomwambia na akawachukua wale watu nyumbani mwa Yusufu. Basi watu hao wakaogopa walipopelekwa nyumbani mwa Yusufu. Wakafikiri, “Tumeletwa hapa kwa ajili ya zile fedha zilizorudishwa katika magunia yetu mara ile ya kwanza. Anataka kutushambulia na kutushinda, atuchukue sisi kama watumwa, na atwae hawa punda wetu.” Hivyo wakamwendea msimamizi wa nyumba wa Yusufu na kuzungumza naye kwenye ingilio la nyumba. Wakasema, “Tafadhali bwana, tulikuja hapa mara ya kwanza kununua chakula. Lakini mahali pale tulipotua wakati wa jioni tulifungua magunia yetu, na kila mmoja wetu akakuta fedha zake katika gunia lake, kiasi kile kile tulicholeta. Kwa hiyo tumezirudisha. Pia tumeleta fedha nyingine kwa ajili ya kununulia chakula. Hatujui ni nani aliziweka fedha hizo katika magunia yetu.” Akawaambia, “Vema, msiogope. Mungu wenu, Mungu wa baba yenu, amewapa ninyi hazina katika magunia yenu; mimi nilipokea fedha yenu.” Ndipo akawaletea Simeoni. Msimamizi akawapeleka wale watu nyumbani mwa Yusufu, akawapa maji ya kunawa miguu, na kuwapa punda wao majani. Wakaandaa zawadi zao ili wampe Yusufu atakapofika adhuhuri, kwa kuwa walikuwa wamesikia kwamba watakula chakula huko. Yusufu alipokuja nyumbani, walimkabidhi zile zawadi ambazo walikuwa wamezileta mle nyumbani, nao wakamsujudia. Akawauliza kuhusu hali yao, kisha akawaambia, “Yule baba yenu mzee mliyeniambia habari zake, yu hali gani? Je, bado yu hai?” Wakamjibu, “Mtumishi wako, baba yetu, bado anaishi na ni mzima.” Kisha wakainama, wakamsujudia.