Mwanzo 43:1-14
Mwanzo 43:1-14 NENO
Wakati huu njaa ilikuwa bado ni kali mno katika nchi. Hivyo wakati walikuwa wamemaliza kula nafaka yote waliyoileta kutoka Misri, baba yao akawaambia, “Rudini Misri mkatununulie chakula kingine.” Lakini Yuda akamwambia, “Mtu yule alituonya kwa msisitizo, ‘Hamtauona uso wangu tena hadi mje na ndugu yenu.’ Kama utakubali ndugu yetu aende pamoja nasi, tutaenda kuwanunulia chakula. Lakini ikiwa hutamruhusu aende, hatutaenda, kwa sababu mtu yule alituambia, ‘Hamtauona uso wangu tena hadi mje na ndugu yenu.’ ” Israeli akauliza, “Kwa nini mkaniletea taabu hii kwa kumwambia yule mtu mlikuwa na ndugu mwingine?” Wakamjibu, “Yule mtu alituhoji kwa undani sana habari zetu na za jamaa yetu. Alituuliza, ‘Je, baba yenu bado angali hai? Je, mnaye ndugu mwingine?’ Sisi tulimjibu maswali yake tu. Tungewezaje kujua kwamba angesema, ‘Mleteni mdogo yenu hapa’?” Ndipo Yuda akamwambia baba yake Israeli, “Mtume kijana pamoja nami, nasi tutaondoka mara moja, ili sisi na wewe pamoja na watoto wetu tuweze kuishi, wala tusife. Mimi mwenyewe nitakuhakikishia usalama wake; mimi mwenyewe nitawajibika kumrudisha. Nisipomrudisha kwako na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye lawama mbele yako maisha yangu yote. Hakika, kama hatukuchelewa kuondoka, tungekuwa tumeenda na kurudi mara mbili.” Basi baba yao Israeli akawaambia, “Kama ni lazima iwe hivyo, basi fanyeni hivi: Wekeni sehemu ya bidhaa bora za nchi katika mifuko yenu, na mmpelekee yule mtu kama zawadi: zeri kidogo, asali kidogo, vikolezo, manemane, kungu na lozi. Chukueni fedha mara mbili, kwa kuwa mtazirudisha zile fedha zilizowekwa midomoni mwa magunia yenu. Labda ziliwekwa kwa makosa. Mchukueni ndugu yenu pia, mrudi kwa huyo mtu mara moja. Naye Mungu Mwenyezi awajalie rehema mbele ya huyo mtu ili apate kumwachia yule ndugu yenu na Benyamini mweze kurudi pamoja. Kwangu mimi, kama nikufiwa, nimefiwa.”