Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 4:8-24

Mwanzo 4:8-24 NENO

Basi Kaini akamwambia ndugu yake Abeli, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Abeli ndugu yake, akamuua. Kisha BWANA akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?” Akamjibu, “Sijui. Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” BWANA akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini. Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako. Utakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu.” Kaini akamwambia BWANA, “Adhabu yangu ni zaidi ya ninavyoweza kustahimili. Leo unanifukuza kutoka nchi, nami nitafichwa mbali na uwepo wako. Nitakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu, na yeyote anionaye ataniua.” Lakini BWANA akamwambia, “La, sivyo! Ikiwa mtu yeyote atamuua Kaini, atalipizwa kisasi mara saba.” Kisha BWANA akamwekea Kaini alama ili yeyote angemwona asimuue. Kwa hiyo Kaini akaondoka mbele za BWANA, akaenda kuishi katika nchi ya Nodi, mashariki mwa Edeni. Kaini akakutana kimwili na mkewe, naye akapata mimba na akamzaa Henoko. Wakati huo Kaini alikuwa anajenga mji, akauita Henoko, jina la mtoto wake. Henoko akamzaa Iradi; Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli; naye Methushaeli akamzaa Lameki. Lameki alioa wanawake wawili: mmoja aliitwa Ada, na mwingine Sila. Ada akamzaa Yabali; huyu akawa baba wa wale wanaoishi katika mahema na kufuga wanyama. Kaka yake aliitwa Yubali, aliyekuwa baba wa wote wapigao zeze na filimbi. Pia Sila alikuwa na mtoto wa kiume aliyeitwa Tubali-Kaini, ambaye alifua vifaa vya aina mbalimbali vya shaba na chuma. Naama alikuwa dada wa Tubali-Kaini. Lameki akawaambia wake zake, “Ada na Sila, nisikilizeni mimi; wake wa Lameki sikieni maneno yangu. Nimemuua mtu kwa kunijeruhi, kijana mdogo kwa kuniumiza. Kama Kaini atalipizwa kisasi mara saba, basi Lameki itakuwa mara sabini na saba.”