Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 4:1-15

Mwanzo 4:1-15 NENO

Adamu akakutana kimwili na mkewe Hawa, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Hawa akasema, “Kwa msaada wa BWANA nimemzaa mtoto wa kiume.” Baadaye akamzaa Abeli ndugu yake. Basi Abeli akawa mfugaji, na Kaini akawa mkulima. Baada ya muda, Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba ikiwa sadaka kwa BWANA. Lakini Abeli akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. BWANA akamkubali Abeli pamoja na sadaka yake, lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni. Kisha BWANA akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni? Ukifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, ikikutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.” Basi Kaini akamwambia ndugu yake Abeli, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Abeli ndugu yake, akamuua. Kisha BWANA akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?” Akamjibu, “Sijui. Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” BWANA akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini. Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako. Utakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu.” Kaini akamwambia BWANA, “Adhabu yangu ni zaidi ya ninavyoweza kustahimili. Leo unanifukuza kutoka nchi, nami nitafichwa mbali na uwepo wako. Nitakuwa mtu wa kutangatanga duniani bila utulivu, na yeyote anionaye ataniua.” Lakini BWANA akamwambia, “La, sivyo! Ikiwa mtu yeyote atamuua Kaini, atalipizwa kisasi mara saba.” Kisha BWANA akamwekea Kaini alama ili yeyote angemwona asimuue.