Mwanzo 28:1-9
Mwanzo 28:1-9 NENO
Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki na akamwamuru, akisema, “Usioe mwanamke Mkanaani. Nenda mara moja hadi Padan-Aramu, kwenye nyumba ya Bethueli, baba wa mama yako. Uchukue mke kati ya binti za Labani ambaye ni ndugu wa mama yako. Mungu Mwenyezi na akubariki, uwe na uzao, uongezeke idadi yako hadi upate kuwa jamii kubwa ya watu. Akupe wewe na uzao wako baraka aliyopewa Abrahamu, upate kumiliki nchi unayoishi sasa kama mgeni, nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu.” Kisha Isaka akamuaga Yakobo, naye akaenda Padan-Aramu, kwa Labani mwana wa Bethueli Mwaramu, ndugu wa Rebeka, mama yao Yakobo na Esau. Basi Esau akajua kuwa Isaka amembariki Yakobo na kumtuma Padan-Aramu ili achukue mke huko, na kwamba alipombariki alimwamuru, akisema, “Usioe mke katika binti za Wakanaani,” tena kwamba Yakobo amewatii baba yake na mama yake, naye ameenda Padan-Aramu. Esau akatambua jinsi baba yake Isaka alivyowachukia binti za Wakanaani. Ndipo Esau akaenda kwa Ishmaeli, akamwoa Mahalati, ndugu wa Nebayothi na binti ya Ishmaeli mwana wa Abrahamu, kuongezea wale wake wengine aliokuwa nao.