Mwanzo 27:21-29
Mwanzo 27:21-29 NENO
Kisha Isaka akamwambia Yakobo, “Mwanangu, tafadhali sogea karibu nami ili nikupapase, nione kama hakika ndiwe Esau mwanangu, au la.” Yakobo akasogea karibu na baba yake Isaka, ambaye alimpapasa na kusema, “Sauti ni ya Yakobo, bali mikono ni ya Esau.” Hakumtambua, kwa sababu mikono yake ilikuwa na nywele kama ya ndugu yake Esau, kwa hiyo akambariki. Akamuuliza, “Kweli wewe ni mwanangu Esau?” Akajibu, “Ni mimi.” Kisha Isaka akasema, “Mwanangu, niletee sehemu ya mawindo yako nile, ili nikubariki.” Yakobo akamletea, naye akala; kisha akamletea na divai akanywa. Ndipo Isaka baba yake akamwambia, “Njoo hapa, mwanangu, unibusu.” Kwa hiyo akamwendea akambusu. Isaka aliposikia harufu ya nguo zake, akambariki, akasema, “Aha, harufu ya mwanangu ni kama harufu ya shamba ambalo BWANA amelibariki. Mungu na akupe umande wa mbinguni na utajiri wa duniani: wingi wa nafaka na divai mpya. Mataifa yakutumikie, na mataifa yakusujudie. Uwe bwana juu ya ndugu zako, na wana wa mama yako wakusujudie. Walaaniwe wale wanaokulaani, na wabarikiwe wale wanaokubariki.”


