Mwanzo 27:1-17
Mwanzo 27:1-17 NENO
Isaka alipokuwa mzee na macho yake yakapofuka kwa kukosa nguvu, akamwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu.” Akajibu, “Mimi hapa.” Isaka akasema, “Mimi sasa ni mzee na sijui siku ya kufa kwangu. Sasa basi chukua silaha zako, podo na upinde, uende nyikani, ukaniwindie mawindo. Uniandalie chakula kitamu nikipendacho uniletee nile, ili nikubariki kabla sijafa.” Rebeka alikuwa akisikiliza Isaka akizungumza na mwanawe Esau. Basi Esau alipoenda nyikani kuwinda mawindo ayalete, Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, “Tazama, nimemsikia baba yako akimwambia ndugu yako Esau, ‘Niletee mawindo, kisha ukaniandalie chakula kitamu nile, ili nikubariki mbele za BWANA kabla sijafa.’ Sasa mwanangu, nisikilize kwa makini na ufanye yale ninayokuambia: Nenda sasa katika kundi ukaniletee wana-mbuzi wawili wazuri, ili nimwandalie baba yako chakula kitamu kile anachokipenda. Kisha umpelekee baba yako ale, ili akubariki kabla hajafa.” Yakobo akamwambia Rebeka mama yake, “Lakini ndugu yangu Esau ana nywele mwilini, nami nina ngozi nyororo. Itakuwaje baba yangu akinigusa? Ataona kama ninamfanyia ujanja, nami nijiletee laana badala ya baraka.” Mama yake akamwambia, “Mwanangu, laana na iwe juu yangu. Fanya tu ninalokuambia: nenda ukaniletee hao wana-mbuzi.” Kwa hiyo alienda akawaleta, akampa mama yake, naye Rebeka akaandaa chakula kitamu, kile alichokipenda baba yake. Kisha Rebeka akachukua nguo nzuri za Esau mwanawe wa kwanza, alizokuwa nazo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. Pia akamfunika mikononi na sehemu laini ya shingo kwa ngozi za mbuzi. Hatimaye akampa Yakobo hicho chakula kitamu pamoja na mkate aliouoka.