Wagalatia 3:1-18
Wagalatia 3:1-18 NENO
Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaroga? Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulubiwa. Nataka nijifunze neno moja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa kushika sheria, au kwa kuyaamini yale mliyosikia? Je, ninyi ni wajinga kiasi hicho? Baada ya kuanza kwa Roho, je, sasa mwataka kumalizia katika mwili? Je, mlipata mateso kiasi hicho bure? Ni kama kweli yalikuwa bure! Je, Mungu huwapa Roho wake na kufanya miujiza kati yenu kwa sababu mnatii sheria, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia? Kama vile “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.” Fahamuni basi kwamba wale walio na imani, hao ndio watoto wa Abrahamu. Andiko liliona tangu awali kwamba Mungu angewahesabia haki watu wa Mataifa kwa imani, hivyo likatangulia kumtangazia Abrahamu Injili, likisema kwamba, “Kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa.” Kwa sababu hii, wale wote wanaoamini wanabarikiwa pamoja na Abrahamu, mtu wa imani. Kwa maana wote wanaotumainia matendo ya sheria wako chini ya laana, kwa kuwa imeandikwa, “Alaaniwe kila mtu asiyeshikilia kutii mambo yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Sheria.” Basi ni dhahiri kwamba hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kushikilia sheria, kwa maana, “Mwenye haki ataishi kwa imani.” Lakini sheria haitegemei imani. Kinyume chake, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” Kristo alitukomboa kutoka laana ya sheria kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikwa, “Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti.” Alitukomboa ili baraka aliyopewa Abrahamu ipate kuwafikia watu wa Mataifa kupitia kwa Kristo Yesu, ili kwa imani tupate kupokea ile ahadi ya Roho. Ndugu zangu, nataka nitoe mfano kutoka maisha ya kila siku. Kama vile hakuna mtu awezaye kutangua au kuongeza kitu katika agano la mtu ambalo limekwisha kuthibitishwa, vivyo hivyo kwa hali kama hii. Ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Maandiko hayasemi “kwa uzao”, yakimaanisha watu wengi, bali “kwa mzao wako”, yaani mtu mmoja, ndiye Kristo. Ninachotaka kusema ni kwamba, sheria, ambayo ilitolewa miaka mia nne na thelathini (430) baadaye, haitangui agano lililothibitishwa na Mungu ili kuibatilisha ahadi ile. Kwa maana kama urithi hupatikana kwa sheria, basi hautegemei tena ahadi, lakini Mungu kwa neema yake alimpa Abrahamu urithi kupitia kwa ahadi.