Ezekieli 40:1-27
Ezekieli 40:1-27 NENO
Katika mwaka wa ishirini na tano wa uhamisho wetu, mwanzoni mwa huo mwaka, siku ya kumi ya mwezi, katika mwaka wa kumi na nne baada ya kuanguka kwa mji, siku hiyo hiyo mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu, naye akanipeleka huko. Nikiwa katika maono ya Mungu alinichukua hadi nchi ya Israeli, naye akaniweka kwenye mlima mrefu sana, ambako upande wa kusini kulikuwa na baadhi ya majengo ambayo yalionekana kama mji. Akanipeleka huko, nami nikamwona mtu ambaye kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwa shaba. Alikuwa amesimama kwenye lango akiwa na kamba ya kitani na ufito wa kupimia mkononi mwake. Mtu huyo akaniambia, “Mwanadamu, fungua macho yako uone, na utege masikio yako usikie, nawe uzingatie yote nitakayokuonesha, kwa kuwa ndiyo sababu umeletwa hapa. Iambie nyumba ya Israeli kila kitu utakachoona.” Nikaona ukuta uliozunguka eneo lote la Hekalu. Ule ufito wa kupimia uliokuwa mkononi mwa yule mtu ulikuwa na urefu wa dhiraa ndefu sita, dhiraa ndefu ikiwa sawa na dhiraa na nyanda nne. Akaupima ule ukuta; ulikuwa na unene wa dhiraa ndefu sita, na kimo cha dhiraa ndefu sita. Kisha akaenda kwenye lango linaloelekea mashariki. Akapanda ngazi zake akapima kizingiti cha lango, nacho kilikuwa na kina cha huo ufito. Vyumba vya kupumzikia vya walinzi vilikuwa na urefu wa huo ufito mmoja na upana wa huo ufito, kuta zilizochomoza kati ya vyumba hivyo vya mapumziko zilikuwa na unene wa dhiraa tano. Nacho kizingiti cha lango lililokuwa karibu na ukumbi unaoelekea hekaluni kilikuwa na kina cha huo ufito. Kisha akapima baraza ya njia ya lango, ambayo ilikuwa na kina cha dhiraa nane na miimo yake ilikuwa na unene wa dhiraa mbili. Baraza ya lango ilielekea Hekalu. Ndani ya lango la mashariki kulikuwepo vyumba vitatu vya kupumzikia kila upande; vyote vitatu vilikuwa na vipimo vilivyo sawa, nazo nyuso za kuta zilizochomoza kila upande zilikuwa na vipimo vilivyo sawa. Kisha akapima upana wa ingilio la lango, ilikuwa dhiraa kumi, na urefu wake ulikuwa dhiraa kumi na tatu. Mbele ya kila chumba cha kupumzikia kulikuwa na ukuta uliokuwa na kimo cha dhiraa moja kwenda juu, navyo hivyo vyumba vilikuwa dhiraa sita mraba. Kisha akapima njia ya lango kuanzia juu ya ukuta wa nyuma wa chumba kimoja cha kupumzikia hadi juu ya ukuta wa nyuma wa chumba upande wa pili; kukawa na nafasi ya dhiraa ishirini na tano kuanzia lango la ukuta mmoja hadi lango la ukuta uliokuwa upande mwingine. Akapima pande za mbele za hizo kuta zilizochomoza kuzunguka hadi ndani ya ingilio. Urefu wake ulikuwa dhiraa sitini. Kipimo kilikuwa hadi baraza iliyoangaliana na ua. Umbali kuanzia ingilio la njia ya lango hadi mwisho kabisa wa baraza yake ulikuwa dhiraa hamsini. Kulikuwa na vidirisha kwenye hivyo vyumba vya walinzi, na nguzo za hivyo vyumba zilikuwa kwenye mzunguko wa hilo lango; vivyo hivyo kulikuwa na madirisha yaliyozunguka kuelekeana na ua. Juu ya kila nguzo kulikuwa na nakshi za mitende. Kisha akanileta katika ukumbi wa nje. Huko nikaona vyumba vingine pamoja na njia iliyokuwa imejengwa kuzunguka ukumbi wote, kulikuwa na vyumba thelathini vimepangana kando ya hiyo njia. Njia hii iliyojengwa iliambaa na lango, ikiwa na urefu sawa na lango; hii ilikuwa ni njia ya chini. Kisha akapima umbali kutoka ndani ya lango la chini mpaka nje ya ukumbi wa ndani, nao ulikuwa dhiraa mia moja upande wa mashariki na dhiraa mia moja upande wa kaskazini. Kisha akapima urefu na upana wa lango linaloelekea kaskazini, kukabili ukumbi wa nje. Vyumba vyake vilikuwa vitatu kila upande, kuta zilizochomoza kati ya vyumba na baraza zilikuwa na vipimo sawa na zile kuta za lango la kwanza. Zilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wa dhiraa ishirini na tano. Madirisha yake, baraza yake na nakshi yake ya mitende vilikuwa na vipimo sawasawa na vile vya lango linaloelekea mashariki. Kulikuwa na ngazi saba za kupandia huko, pamoja na baraza yake mkabala nazo. Kulikuwa na lango kwenye ukumbi wa ndani lililoelekea lile lango la kaskazini, kama vile ilivyokuwa ule upande wa mashariki. Akapima kutoka lango moja hadi lile lililo mkabala nalo, lilikuwa dhiraa mia moja. Ndipo akaniongoza mpaka upande wa kusini, nami nikaona lango linaloelekea kusini. Akaipima miimo yake na baraza yake, navyo vilikuwa na vipimo sawa kama hivyo vingine. Lango na baraza yake vilikuwa na madirisha membamba pande zote, kama madirisha ya huko kwingine. Ilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano. Kulikuwa na ngazi saba za kupandia huko, pamoja na baraza yake mkabala nazo. Ilikuwa na nakshi za mitende kwenye kuta zilizochomoza kati ya vyumba kila upande. Ukumbi wa ndani pia ulikuwa na lango lililoelekea kusini. Naye akapima kutoka lango hili hadi kwenye lango la nje upande wa kusini; ilikuwa dhiraa mia moja.


