Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 32:1-16

Ezekieli 32:1-16 NENO

Katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kumi na mbili, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema: “Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Farao mfalme wa Misri na umwambie: “ ‘Wewe ni kama simba miongoni mwa mataifa, wewe ni kama mnyama mkubwa baharini, unapiga maji kwa kishindo katika vijito vyako, unayavuruga maji kwa miguu yako, na kuchafua vijito. “ ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: “ ‘Nikiwa pamoja na wingi mkubwa wa watu nitautupa wavu wangu juu yako, nao watakukokota katika wavu wangu. Nitakutupa nchi kavu na kukuvurumisha uwanjani. Nitawafanya ndege wote wa angani watue juu yako na wanyama wote wa nchi watajishibisha nyama yako. Nitatawanya nyama yako juu ya milima na kujaza mabonde kwa mabaki yako. Nitailowanisha nchi kwa damu yako inayotiririka njia yote hadi milimani, nayo mabonde yatajazwa na nyama yako. Nitakapokuzimisha, nitafunika mbingu na kuzitia nyota zake giza; nitalifunika jua kwa wingu, nao mwezi hautatoa nuru yake. Mianga yote itoayo nuru angani nitaitia giza juu yako; nitaleta giza juu ya nchi yako, asema BWANA Mwenyezi. Nitaifadhaisha mioyo ya mataifa mengi nitakapokuangamiza miongoni mwa mataifa, nikikuleta uhamishoni miongoni mwa nchi ambazo hujapata kuzijua. Nitayafanya mataifa mengi wakustaajabie, wafalme wao watatetemeka kwa hofu kwa ajili yako nitakapotikisa upanga wangu mbele yao. Siku ya anguko lako kila mmoja wao atatetemeka kila dakika kwa ajili ya maisha yake. “ ‘Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: “ ‘Upanga wa mfalme wa Babeli utakuja dhidi yako. Nitayafanya makundi yako kuanguka kwa panga za mashujaa: taifa katili kuliko mataifa yote. Watakivunjavunja kiburi cha Misri, nayo makundi yake yote yatashindwa. Nitaangamiza mifugo yake yote wanaojilisha kando ya maji mengi: hayatavurugwa tena kwa mguu wa mwanadamu wala kwato za mnyama hazitayachafua tena. Kisha nitafanya maji yake yatulie na kufanya vijito vyake vitiririke kama mafuta, asema BWANA Mwenyezi. Nitakapoifanya Misri kuwa ukiwa, na kuiondolea nchi kila kitu kilichomo, nitakapowapiga wote wanaoishi humo, ndipo watajua kuwa Mimi ndimi BWANA.’ “Hili ndilo ombolezo watakalomwimbia. Binti za mataifa wataliimba, kwa kuwa Misri na makundi yake yote wataliimba, asema BWANA Mwenyezi.”