Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 22:1-22

Ezekieli 22:1-22 NENO

Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, je, wewe utauhukumu? Je, utauhukumu huu mji unaomwaga damu? Basi uujulishe kuhusu matendo yake yote ya machukizo uuambie: ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: Ee mji unaojiletea maangamizi wenyewe kwa kumwaga damu ndani yake na kujinajisi wenyewe kwa kutengeneza sanamu, umekuwa na hatia kwa sababu ya damu uliyomwaga, na umetiwa unajisi kwa sanamu ulizotengeneza. Umejiletea mwisho wa siku zako na mwisho wa miaka yako umewadia. Kwa hiyo nitakufanya kitu cha kudharauliwa kwa mataifa na kitu cha mzaha kwa nchi zote. Wale walio karibu na wale walio mbali watakudhihaki, ewe mji wenye sifa mbaya, uliyejaa ghasia. “ ‘Tazama jinsi kila mkuu wa Israeli aliye ndani yako anavyotumia nguvu zake kumwaga damu. Ndani yako wamewadharau baba na mama; ndani yako wamewatendea wageni udhalimu, na kuwadhulumu yatima na wajane. Mmedharau vitu vyangu vitakatifu na kuzinajisi Sabato zangu. Ndani yako wako watu wasingiziaji, watu walio tayari kumwaga damu, ndani yako wako wale wanaokula vyakula vilivyotolewa mahali pa ibada za sanamu kwenye milima, na kutenda matendo ya uasherati. Ndani yako wako wale wanaovunjia heshima vitanda vya baba zao, ndani yako wamo wale wanaowatendea wanawake jeuri wakiwa katika hedhi, wakati wakiwa najisi. Ndani yako mtu hufanya mambo ya machukizo na mke wa jirani yake, mwingine kwa aibu kubwa hukutana kimwili na mke wa mwanawe, mwingine humtenda jeuri dada yake, binti ya baba yake hasa. Ndani yako watu hupokea rushwa ili kumwaga damu, mnapokea riba na faida ya ziada na kupata faida isiyokuwa halali kutoka kwa majirani ili kupata faida kubwa kupita kiasi. Nawe umenisahau mimi, asema BWANA Mwenyezi. “ ‘Hakika nitapiga makofi kwa ajili ya faida isiyo halali uliyojipatia na kwa damu uliyoimwaga ndani yako. Je, ujasiri wako utadumu au mikono yako itakuwa na nguvu siku hiyo nitakapokuadhibu? Mimi BWANA nimesema na nitalifanya. Nitakutawanya miongoni mwa mataifa na kukutapanya katika nchi mbalimbali nami nitakomesha unajisi wako. Baada ya kunajisika mbele ya mataifa, utajua kuwa Mimi ndimi BWANA.’ ” Ndipo neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, nyumba ya Israeli imekuwa takataka ya chuma kwangu; wote wamekuwa shaba, bati, chuma na risasi iliyoachwa kalibuni. Wao ni taka ya madini ya fedha tu. Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: ‘Kwa kuwa wote mmekuwa takataka ya chuma, nitawakusanya Yerusalemu. Kama vile watu wakusanyavyo fedha, shaba, chuma, risasi na bati kalibuni ili kuyeyusha kwa moto mkali, ndivyo nitakavyowakusanya katika hasira yangu na ghadhabu yangu kuwaweka ndani ya mji na kuwayeyusha. Nitawakusanya na kupuliza juu yenu moto wa hasira yangu na ghadhabu yangu nanyi mtayeyushwa ndani ya huo mji. Kama fedha iyeyukavyo kalibuni, ndivyo mtakavyoyeyuka ndani ya huo mji, nanyi mtajua kuwa Mimi, BWANA, nimemwaga ghadhabu yangu juu yenu.’ ”