Kutoka 8:20-32
Kutoka 8:20-32 NENO
Kisha BWANA akamwambia Musa, “Amka asubuhi na mapema, usimame mbele ya Farao wakati anapoenda mtoni, umwambie, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu. Usipowaruhusu watu wangu waondoke, nitatuma makundi ya inzi juu yako na maafisa wako, juu ya watu wako, na ndani ya nyumba zenu. Nyumba za Wamisri zitajaa inzi; hata ardhi itafunikwa na inzi. “ ‘Lakini siku ile nitafanya kitu tofauti katika nchi ya Gosheni, ambapo watu wangu wanaishi, hapatakuwa na makundi ya inzi, ili mpate kujua kwamba Mimi, BWANA, niko katika nchi hii. Nitaweka tofauti kati ya watu wangu na watu wenu. Ishara hii ya ajabu itatokea kesho.’ ” Naye BWANA akafanya hivyo. Makundi makubwa ya inzi walimiminika katika jumba la kifalme la Farao na katika nyumba za maafisa wake, pia nchi yote ya Misri ikaharibiwa na inzi. Ndipo Farao akamwita Musa na Haruni na kuwaambia, “Nendeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu katika nchi hii.” Lakini Musa akamwambia, “Hilo halitakuwa sawa. Dhabihu tutakazomtolea BWANA Mungu wetu zitakuwa chukizo kwa Wamisri. Tukitoa dhabihu ambazo ni chukizo mbele yao, je, hawatatupiga mawe? Ni lazima twende mwendo wa siku tatu hadi tufike jangwani ili tumtolee BWANA Mungu wetu dhabihu, kama alivyotuagiza.” Farao akamwambia, “Nitawaruhusu mwende kumtolea BWANA Mungu wenu dhabihu huko jangwani, lakini hamna ruhusa kwenda mbali sana. Sasa mniombee.” Musa akajibu, “Mara tu nitakapoondoka, nitamwomba BWANA na kesho inzi wataondoka kwa Farao, kwa maafisa wake, na kwa watu wake. Ila hakikisha kwamba Farao hatatenda kwa udanganyifu tena kwa kutokuwaachia watu waende kumtolea BWANA dhabihu.” Ndipo Musa akamwacha Farao na kumwomba BWANA, naye BWANA akafanya lile Musa alilomwomba. Inzi wakaondoka kwa Farao, kwa maafisa wake na kwa watu wake, wala hakuna hata inzi aliyebakia. Lakini wakati huu pia Farao akaufanya moyo wake kuwa mgumu, wala hakuwaruhusu Waisraeli waondoke.