Kutoka 7:14-25
Kutoka 7:14-25 NENO
Kisha BWANA akamwambia Musa, “Moyo wa Farao ni mgumu; anakataa kuwaacha watu waondoke. Nenda kwa Farao asubuhi anapoenda mtoni. Ngoja ukingoni mwa Mto Naili ili uonane naye, na uchukue mkononi mwako fimbo ile iliyobadilishwa kuwa nyoka. Kisha umwambie, ‘BWANA, Mungu wa Waebrania, amenituma nikuambie: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu jangwani. Lakini hadi sasa hujasikiliza. Hili ndilo asemalo BWANA: Kwa hili utajua kuwa Mimi ndimi BWANA: Kwa fimbo iliyo mkononi mwangu nitapiga maji ya Mto Naili, nayo yatabadilika kuwa damu. Samaki walio katika Mto Naili watakufa, nao mto utanuka vibaya; Wamisri hawataweza kunywa maji yake.’ ” BWANA akamwambia Musa, “Mwambie Haruni, ‘Chukua ile fimbo yako unyooshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya chemchemi na mifereji, juu ya madimbwi na mabwawa yote,’ navyo vitabadilika kuwa damu. Damu itakuwa kila mahali katika Misri, hata kwenye vyombo vya miti na vya mawe.” Musa na Haruni wakafanya kama vile BWANA alivyokuwa amewaagiza. Akainua fimbo yake machoni pa Farao na maafisa wake na kuyapiga maji ya Mto Naili, na maji yote yakabadilika kuwa damu. Samaki katika Mto Naili wakafa, nao mto ukanuka vibaya sana kiasi kwamba Wamisri hawakuweza kunywa maji yake. Damu ilikuwa kila mahali katika nchi ya Misri. Lakini waganga wa Misri kwa kutumia siri ya uganga wao wakafanya vivyo hivyo, nao moyo wa Farao ukawa mgumu, hakuwasikiliza Musa na Haruni, kama vile BWANA alivyokuwa amesema. Badala yake, Farao akageuka, akaenda kwenye jumba lake la kifalme, wala hakulitia hili moyoni. Nao Wamisri wote wakachimba kandokando ya Mto Naili kupata maji ya kunywa, kwa sababu hawakuweza kunywa maji ya mto. Zilipita siku saba baada ya BWANA kuyapiga maji ya Mto Naili.