Kutoka 31
31
Bezaleli na Oholiabu
(Kut 35:30–36:1)
1Ndipo Bwana akamwambia Musa, 2“Tazama, nimemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, 3nami nimemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, uwezo na ujuzi katika aina zote za ufundi, 4ili kubuni michoro ya kupendeza katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba, 5kuchonga vito na kuvitia mahali, kufanya ufundi kwa mbao, na kujishughulisha na aina zote za ufundi. 6Tena nimemteua Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, ili kumsaidia.
“Pia mafundi wote nimewapa ustadi wa kutengeneza kila kitu nilichokuamuru wewe:
7“Hema la Kukutania,
Sanduku la Ushuhuda pamoja na kiti cha rehema juu yake,
pia na vifaa vyote vya kwenye hema:
8meza na vifaa vyake,
kinara cha taa cha dhahabu safi na vifaa vyake vyote,
madhabahu ya kufukizia uvumba,
9madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote,
sinia na kinara chake,
10pamoja na mavazi matakatifu yaliyofumwa ya kuhani Haruni,
na mavazi kwa ajili ya wanawe wakati wanahudumu katika kazi ya ukuhani,
11pia mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri kwa ajili ya Mahali Patakatifu.
“Watavitengeneza jinsi nilivyokuagiza.”
Sabato
12Kisha Bwana akamwambia Musa, 13“Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni lazima mzishike Sabato zangu. Hii itakuwa ni ishara kati yangu na ninyi kwa vizazi vijavyo, ili mpate kujua kwamba Mimi Ndimi Bwana, niwafanyaye ninyi watakatifu.
14“ ‘Mtaishika Sabato, kwa sababu ni takatifu kwenu. Yeyote atakayeinajisi lazima auawe, yeyote atakayefanya kazi siku hiyo lazima akatiliwe mbali na watu wake. 15Kwa siku sita, mtafanya kazi, lakini siku ya saba ni Sabato ya mapumziko, takatifu kwa Bwana. Yeyote afanyaye kazi yoyote siku ya Sabato ni lazima auawe. 16Waisraeli wataishika Sabato, kuiadhimisha kwa vizazi vijavyo kuwa agano la milele. 17Itakuwa ishara kati yangu na Waisraeli milele, kwa kuwa kwa muda wa siku sita Bwana aliumba mbingu na dunia, akapumzika siku ya saba, akastarehe.’ ”
18 Bwana alipomaliza kusema na Musa juu ya Mlima Sinai, Mungu akampa vile vibao viwili vya Ushuhuda, vibao vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu.
Iliyochaguliwa sasa
Kutoka 31: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.