Kutoka 16:9-26
Kutoka 16:9-26 NENO
Kisha Musa akamwambia Haruni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli kwamba, ‘Mje mbele zake BWANA, kwa maana amesikia manungʼuniko yenu.’ ” Haruni alipokuwa akizungumza na jumuiya yote ya Waisraeli, wakatazama kuelekea jangwani, na huko wakaona utukufu wa BWANA ukitokeza katika wingu. BWANA akamwambia Musa, “Nimesikia manungʼuniko ya Waisraeli. Waambie, ‘Jioni mtakula nyama, na asubuhi mtashiba mikate. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.’ ” Jioni ile kware wakaja wakaifunika kambi na asubuhi kulikuwa na utando wa umande kuzunguka kambi. Umande ulipoondoka, vipande vidogo vidogo kama theluji vilionekana juu ya mchanga wa jangwa. Waisraeli walipoona, wakaambiana, “Hiki ni nini?” Kwa kuwa hawakujua kilikuwa kitu gani. Musa akawaambia, “Huu ndio mkate ambao BWANA amewapa mle. Hivi ndivyo BWANA ameamuru: ‘Kila mmoja akusanye kiasi anachohitaji. Chukueni pishi moja kwa kila mtu mliye naye katika hema lenu.’ ” Waisraeli wakafanya kama walivyoambiwa; baadhi yao wakakusanya zaidi, wengine pungufu. Nao walipopima katika pishi, yule aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa. Kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji. Kisha Musa akawaambia, “Mtu yeyote asibakize chochote hadi asubuhi.” Hata hivyo, wengine hawakuzingatia aliyosema Musa, wakahifadhi kiasi fulani hadi asubuhi, lakini kile alichohifadhi kikajaa mabuu na kuanza kunuka. Kwa hiyo Musa akawakasirikia. Kila asubuhi, kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji na jua lilipokuwa kali, iliyeyuka. Siku ya sita, wakakusanya mara mbili, kiasi cha pishi mbili kwa kila mtu, nao viongozi wa jumuiya wakaja kumwarifu Musa. Musa akawaambia, “Hivi ndivyo alivyoagiza BWANA: ‘Kesho itakuwa Sabato ya mapumziko, Sabato takatifu kwa BWANA. Kwa hiyo okeni kile mnachotaka kuoka na mchemshe kile mnachotaka kuchemsha. Hifadhini chochote kinachobaki na mkiweke hadi asubuhi.’ ” Kwa hiyo wakavihifadhi hadi asubuhi, kama Musa alivyoagiza, na havikunuka wala kuwa na mabuu. Musa akawaambia, “Kuleni leo, kwa sababu leo ni Sabato kwa BWANA. Hamtapata chochote juu ya nchi leo. Kwa siku sita mtakusanya, lakini siku ya saba, yaani Sabato, hakutakuwa chochote.”