Kutoka 16:1-8
Kutoka 16:1-8 NENO
Jumuiya yote ya Waisraeli wakaondoka Elimu, wakafika Jangwa la Sini, lililokuwa kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka Misri. Huko jangwani, jumuiya yote wakawanungʼunikia Musa na Haruni. Waisraeli wakawaambia, “Laiti tungekufa kwa mkono wa BWANA huko Misri! Huko tuliketi tukizunguka masufuria ya nyama na tukala vyakula tulivyovitaka, lakini ninyi mmetuleta huku jangwani ili mpate kuua mkutano huu wote kwa njaa.” Kisha BWANA akamwambia Musa, “Tazama! Nitawanyeshea mikate kutoka mbinguni. Watu watatoka kila siku na kukusanya kitakachowatosha kwa siku ile, kwa njia hii, nitawajaribu nione kama watafuata maelekezo yangu. Siku ya sita watatayarisha kile waletacho ndani, nacho kitakuwa mara mbili kuliko ya kile walichokusanya kila siku.” Kwa hiyo Musa na Haruni wakawaambia Waisraeli wote, “Jioni mtajua kuwa BWANA ndiye aliwatoa Misri, kisha asubuhi mtauona utukufu wa BWANA, kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani hata mtunungʼunikie?” Kisha Musa akasema, “Mtajua kuwa alikuwa BWANA wakati atakapowapa nyama mle ifikapo jioni na mikate yote mtakayohitaji asubuhi kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani? Hamnungʼuniki dhidi yetu, bali dhidi ya BWANA.”