Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 16:1-18

Kutoka 16:1-18 NENO

Jumuiya yote ya Waisraeli wakaondoka Elimu, wakafika Jangwa la Sini, lililokuwa kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka Misri. Huko jangwani, jumuiya yote wakawanungʼunikia Musa na Haruni. Waisraeli wakawaambia, “Laiti tungekufa kwa mkono wa BWANA huko Misri! Huko tuliketi tukizunguka masufuria ya nyama na tukala vyakula tulivyovitaka, lakini ninyi mmetuleta huku jangwani ili mpate kuua mkutano huu wote kwa njaa.” Kisha BWANA akamwambia Musa, “Tazama! Nitawanyeshea mikate kutoka mbinguni. Watu watatoka kila siku na kukusanya kitakachowatosha kwa siku ile, kwa njia hii, nitawajaribu nione kama watafuata maelekezo yangu. Siku ya sita watatayarisha kile waletacho ndani, nacho kitakuwa mara mbili kuliko ya kile walichokusanya kila siku.” Kwa hiyo Musa na Haruni wakawaambia Waisraeli wote, “Jioni mtajua kuwa BWANA ndiye aliwatoa Misri, kisha asubuhi mtauona utukufu wa BWANA, kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani hata mtunungʼunikie?” Kisha Musa akasema, “Mtajua kuwa alikuwa BWANA wakati atakapowapa nyama mle ifikapo jioni na mikate yote mtakayohitaji asubuhi kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani? Hamnungʼuniki dhidi yetu, bali dhidi ya BWANA.” Kisha Musa akamwambia Haruni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli kwamba, ‘Mje mbele zake BWANA, kwa maana amesikia manungʼuniko yenu.’ ” Haruni alipokuwa akizungumza na jumuiya yote ya Waisraeli, wakatazama kuelekea jangwani, na huko wakaona utukufu wa BWANA ukitokeza katika wingu. BWANA akamwambia Musa, “Nimesikia manungʼuniko ya Waisraeli. Waambie, ‘Jioni mtakula nyama, na asubuhi mtashiba mikate. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.’ ” Jioni ile kware wakaja wakaifunika kambi na asubuhi kulikuwa na utando wa umande kuzunguka kambi. Umande ulipoondoka, vipande vidogo vidogo kama theluji vilionekana juu ya mchanga wa jangwa. Waisraeli walipoona, wakaambiana, “Hiki ni nini?” Kwa kuwa hawakujua kilikuwa kitu gani. Musa akawaambia, “Huu ndio mkate ambao BWANA amewapa mle. Hivi ndivyo BWANA ameamuru: ‘Kila mmoja akusanye kiasi anachohitaji. Chukueni pishi moja kwa kila mtu mliye naye katika hema lenu.’ ” Waisraeli wakafanya kama walivyoambiwa; baadhi yao wakakusanya zaidi, wengine pungufu. Nao walipopima katika pishi, yule aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa. Kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji.

Video ya Kutoka 16:1-18