Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Esta 9:1-16

Esta 9:1-16 NENO

Katika siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari, amri iliyoagizwa na mfalme ilikuwa itekelezwe. Siku hii adui wa Wayahudi walikuwa wametumaini kuwashinda, lakini sasa mambo yaliwageukia na Wayahudi wakawashinda wale waliokuwa wanawachukia. Wayahudi walikusanyika katika miji yao, katika majimbo ya Mfalme Ahasuero kuwashambulia wale waliokuwa wanatafuta kuwaangamiza. Hakuna yeyote aliyeweza kushindana nao, kwa sababu watu wa mataifa mengine yote waliwaogopa. Nao wakuu wote wa majimbo, majemadari, watawala na maafisa wa mfalme wakawasaidia Wayahudi, kwa sababu walimhofu Mordekai. Mordekai alikuwa mtu mashuhuri katika jumba la mfalme; sifa zake zilienea katika majimbo yote naye alipata uwezo zaidi na zaidi. Wayahudi waliwaangusha adui zao wote kwa upanga wakiwaua na kuwaangamiza, nao walifanya kile walichotaka kwa wale waliowachukia. Katika ngome ya Shushani Wayahudi waliua na kuangamiza wanaume mia tano. Pia waliwaua Parshendatha, Dalfoni, Aspatha, Poratha, Adalia, Ardatha, Parmashta, Arisai, Aridai na Waizatha, wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui wa Wayahudi. Lakini hawakuchukua nyara. Mfalme aliarifiwa siku hiyo hiyo hesabu ya waliouawa katika ngome ya Shushani. Mfalme akamwambia Malkia Esta, “Wayahudi wamewaua wanaume mia tano, na wana kumi wa Hamani ndani ya ngome ya Shushani. Wamefanyaje katika majimbo mengine ya mfalme yaliyobaki? Je, sasa haja yako ni nini? Nayo pia utapewa. Nalo ombi lako ni nini? Nalo utatendewa.” Esta akajibu, “Ikimpendeza mfalme, uwape ruhusa Wayahudi walio Shushani warudie amri ya leo kesho pia, na wana wa Hamani kumi wanyongwe mahali pa kunyongea watu.” Basi mfalme akaamuru kwamba hili litendeke. Amri ilitolewa huko Shushani, nao wakawanyonga wana kumi wa Hamani. Wayahudi huko Shushani wakakusanyika pamoja siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, nao wakawaua wanaume mia tatu huko Shushani, lakini hawakuchukua nyara zao. Wakati ule ule, Wayahudi wengine waliokuwa kwenye majimbo ya mfalme, wakakusanyika kujilinda nao wakapata nafuu kutokana na adui zao. Waliua adui zao wapatao elfu sabini na tano, lakini hawakugusa nyara zao.