Danieli 5:1-16
Danieli 5:1-16 NENO
Mfalme Belshaza aliandaa karamu kubwa kwa ajili ya wakuu wake elfu moja, na akanywa mvinyo pamoja nao. Belshaza alipokuwa akinywa divai, aliamuru vile vikombe vya dhahabu na fedha ambavyo Nebukadneza baba yake alikuwa amevichukua kutoka hekalu huko Yerusalemu viletwe, ili mfalme na wakuu wake, pamoja na wake zake na masuria wake wapate kuvinywea. Kwa hiyo wakavileta vile vikombe vya dhahabu ambavyo vilikuwa vimechukuliwa kutoka hekalu la Mungu huko Yerusalemu, naye mfalme na wakuu wake, pamoja na wake zake na masuria wake wakavinywea. Walipokuwa wakinywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu na fedha, ya shaba, chuma, miti na mawe. Ghafula vidole vya mkono wa mwanadamu vilitokea na kuandika juu ya chokaa ya ukuta, karibu na kinara cha taa ndani ya jumba la mfalme. Mfalme akatazama kitanga kilivyokuwa kikiandika. Uso wa mfalme ukageuka rangi, naye akaogopa sana, kiasi kwamba magoti yake yaligongana na miguu yake ikalegea. Mfalme akawaita wasihiri, wanajimu na waaguzi waletwe, naye akawaambia hao wenye hekima wa Babeli, “Yeyote asomaye maandishi haya na kuniambia maana yake atavikwa nguo za zambarau, na kuvikwa mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atafanywa mtawala wa cheo cha tatu katika ufalme.” Ndipo wenye hekima wote wa mfalme wakaingia, lakini hawakuweza kusoma yale maandishi wala kumwambia mfalme maana yake. Basi Mfalme Belshaza akazidi kujawa na hofu, na uso wake ukageuka rangi zaidi. Wakuu wake wakapigwa na bumbuazi. Malkia aliposikia sauti za mfalme na wakuu wake, alikuja katika ukumbi wa karamu. Akasema, “Ee mfalme, uishi milele! Usishtuke! Usibadilike rangi hivyo! Yuko mtu katika ufalme wako mwenye roho ya miungu mitakatifu ndani yake. Wakati wa baba yako, mtu huyo alionekana kuwa na ufahamu, akili na hekima kama ile ya miungu. Mfalme Nebukadneza baba yako, naam, mfalme baba yako, alimweka kuwa mkuu wa waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi. Mtu huyu Danieli, ambaye mfalme alimwita Belteshaza, alionekana kuwa na akili nyepesi, maarifa na ufahamu, pia uwezo wa kufasiri ndoto, kueleza mafumbo, na kutatua matatizo magumu. Mwite Danieli, naye atakuambia maana ya haya maandishi.” Hivyo Danieli akaletwa mbele ya mfalme, naye mfalme akamuuliza, “Je, wewe ndiwe Danieli, mmoja wa watu wa uhamisho walioletwa na mfalme baba yangu kutoka Yuda? Nimesikia kwamba roho ya miungu iko ndani yako, na kwamba una ufahamu, akili na hekima ya pekee. Watu wenye hekima na wasihiri waliletwa mbele yangu ili kusoma maandishi haya na kuniambia maana yake, lakini hawakuweza kunifafanulia. Basi nimesikia kwamba unaweza kutoa tafsiri na kutatua matatizo magumu. Ikiwa unaweza kusoma maandishi haya na kuniambia maana yake, utavikwa nguo za zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni mwako, nawe utafanywa mtawala wa tatu katika ufalme.”