Danieli 3:1-18
Danieli 3:1-18 NENO
Mfalme Nebukadneza alitengeneza sanamu ya dhahabu, yenye kimo cha dhiraa sitini, na upana wa dhiraa sita, akaisimamisha kwenye tambarare ya Dura katika jimbo la Babeli. Kisha mfalme akaita wakuu, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, waamuzi, mahakimu, na maafisa wengine wote wa jimbo kuja kuizindua sanamu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha. Basi wakuu, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, waamuzi, mahakimu, na maafisa wengine wote wa jimbo wakakusanyika ili kuizindua sanamu ile Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha, nao wakasimama mbele ya hiyo sanamu. Ndipo mpiga mbiu akatangaza kwa sauti kubwa, “Enyi watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha, hili ndilo mnaloamriwa kulifanya: Mara mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari, na aina zote za sauti za ala za uimbaji, lazima msujudu na kuabudu sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza ameisimamisha. Mtu ambaye hataanguka chini na kuiabudu sanamu hiyo, atatupwa saa hiyo hiyo ndani ya tanuru linalowaka moto.” Kwa hiyo, mara waliposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari, na aina zote za sauti za ala za uimbaji, watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha wakasujudu na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha. Wakati huo baadhi ya Wakaldayo walijitokeza na kuwashtaki Wayahudi. Wakamwambia Mfalme Nebukadneza, “Ee mfalme, uishi milele! Ee mfalme, umetoa amri kwamba kila mmoja atakayesikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari, na aina zote za sauti za ala za uimbaji, lazima asujudu na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu, na kwamba yeyote ambaye hatasujudu na kuiabudu atatupwa saa hiyo hiyo ndani ya tanuru linalowaka moto. Lakini wako baadhi ya Wayahudi ambao umewaweka juu ya mambo ya jimbo la Babeli, yaani Shadraki, Meshaki na Abednego, ambao hawakujali wewe, ee mfalme. Hawaitumikii miungu yako wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.” Mfalme Nebukadneza, akiwa amekasirika na mwenye ghadhabu kali, akawaita Shadraki, Meshaki na Abednego. Hivyo watu hawa wakaletwa mbele ya mfalme, naye Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba ninyi Shadraki, Meshaki na Abednego hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi wakati mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari na aina zote za ala za uimbaji, kama mtakuwa tayari kusujudu na kuiabudu hiyo sanamu niliyoitengeneza, vyema sana. Lakini kama hamtaiabudu, mtatupwa saa hiyo hiyo ndani ya tanuru linalowaka moto. Naye ni mungu yupi ataweza kuwaokoa ninyi kutoka mkononi mwangu?” Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, hatuhitaji kujitetea mbele zako kuhusu jambo hili. Ikiwa tutatupwa ndani ya tanuru linalowaka moto, Mungu tunayemtumikia anaweza kutuokoa na moto, naye atatuokoa kutoka mkononi mwako, ee mfalme. Lakini hata ikiwa hatatuokoa, ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”