Matendo 10:9-23
Matendo 10:9-23 NENO
Siku iliyofuata, walipokuwa wanaukaribia mji, yapata saa sita mchana, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba. Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana. Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama kitambaa kikubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne. Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani. Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.” Petro akajibu, “La hasha, Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.” Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.” Jambo hili lilitokea mara tatu, na ghafula kile kitambaa kikarudishwa mbinguni. Petro alipokuwa akisumbuka kuhusu maana ya maono hayo, wale watu waliotumwa na Kornelio waliipata nyumba ya Simoni, wakasimama kwenye lango. Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo. Wakati Petro akiwa anafikiria kuhusu yale maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Simoni, kuna watu watatu wanaokutafuta. Inuka na ushuke, usisite kwenda nao kwa kuwa mimi nimewatuma.” Petro akashuka na kuwaambia wale watu waliokuwa wametumwa kutoka kwa Kornelio, “Mimi ndiye mnayenitafuta. Mmekuja kwa sababu gani?” Wale watu wakamjibu, “Tumetumwa na Kornelio yule jemadari. Yeye ni mtu mwema anayemcha Mungu, na anaheshimiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagizwa na malaika mtakatifu akukaribishe nyumbani mwake, ili asikilize maneno utakayomwambia.” Basi Petro akawakaribisha ndani wawe wageni wake. Kesho yake akaondoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu kutoka Yafa wakafuatana naye.