2 Samweli 6:11-23
2 Samweli 6:11-23 NENO
Sanduku la BWANA likakaa katika nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti, kwa miezi mitatu, naye BWANA akambariki pamoja na nyumba yake yote. Kisha Mfalme Daudi akaambiwa, “BWANA ameibariki nyumba ya Obed-Edomu pamoja na kila alicho nacho, kwa sababu ya Sanduku la Mungu.” Basi Daudi akateremka na kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka nyumba ya Obed-Edomu hadi Mji wa Daudi kwa shangwe. Wale waliokuwa wamebeba Sanduku la BWANA walipotembea hatua sita, Daudi alitoa dhabihu fahali na ndama aliyenoneshwa. Daudi, akiwa amevaa kizibau cha kitani, alicheza mbele za BWANA kwa nguvu zake zote, wakati yeye na nyumba yote ya Israeli walipopandisha Sanduku la BWANA kwa shangwe na sauti za tarumbeta. Sanduku la BWANA lilipokuwa linaingia Mji wa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani. Naye alipomwona Mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele za BWANA, akamdharau moyoni mwake. Wakaleta Sanduku la BWANA na kuliweka mahali pake ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimamisha kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za BWANA. Baada ya kumaliza kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, Daudi akawabariki watu katika jina la BWANA wa majeshi. Kisha akatoa mkate, andazi la tende na andazi la zabibu kavu kwa kila mtu katika mkutano wote wa Waisraeli, wanaume kwa wanawake. Nao watu wote wakaenda nyumbani. Daudi aliporudi ili kuwabariki watu wa nyumbani mwake, Mikali binti Sauli akatoka nje kumlaki, akamwambia, “Tazama jinsi mfalme wa Israeli alivyojibainisha mwenyewe leo kwa kuvua mavazi yake machoni pa vijakazi wa watumishi wake, vile mtu asiye na adabu angefanya!” Daudi akamwambia Mikali, “Nilifanya hivyo mbele za BWANA ambaye alinichagua mimi badala ya baba yako au mwingine yeyote kutoka nyumba yake aliponiweka niwe mtawala wa Israeli, watu wa BWANA. Kwa hiyo nitacheza mbele za BWANA. Nitakuwa asiye na heshima kuliko sasa, nami nitajishusha machoni pangu mwenyewe. Lakini kwa hawa vijakazi uliosema habari zao nitaheshimiwa.” Naye Mikali binti Sauli hakuwa na watoto hadi siku ya kufa kwake.