2 Samweli 3:1-21
2 Samweli 3:1-21 NENO
Vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi vilidumu kwa muda mrefu. Daudi akaendelea kuwa imara zaidi na zaidi, wakati nyumba ya Sauli iliendelea kudhoofika zaidi na zaidi. Wana walizaliwa kwa Daudi huko Hebroni: Mzaliwa wake wa kwanza alikuwa Amnoni mwana wa Ahinoamu wa Yezreeli; mzaliwa wake wa pili alikuwa Danieli mwana wa Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli; wa tatu, Absalomu mwana wa Maaka, binti Talmai mfalme wa Geshuri; wa nne, Adoniya mwana wa Hagithi; wa tano, Shefatia mwana wa Abitali; wa sita, Ithreamu mwana wa Egla, mkewe Daudi. Hawa ndio waliozaliwa kwa Daudi huko Hebroni. Wakati wa vita kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi, Abneri alikuwa anajiimarisha katika nafasi yake kwenye nyumba ya Sauli. Basi Sauli alikuwa na suria, jina lake Rispa binti Aya. Naye Ish-Boshethi akamwambia Abneri, “Kwa nini umekutana kimwili na suria wa baba yangu?” Abneri akakasirika sana kwa sababu ya kile Ish-Boshethi alichosema, naye akamjibu, “Je, mimi ni kichwa cha mbwa, kwa upande wa Yuda? Siku hii ya leo mimi ni mtiifu kwa nyumba ya baba yako Sauli, kwa jamaa yake na rafiki zake. Sijakukabidhi kwa Daudi, lakini bado unanilaumu kwa kosa la kuhusika na huyu mwanamke! Mungu na amwadhibu Abneri vikali zaidi ikiwa sitafanya kwa ajili ya Daudi kile BWANA alichomwahidi kwa kiapo, na kuuhamisha ufalme kutoka nyumba ya Sauli na kuimarisha kiti cha ufalme cha Daudi juu ya Israeli na Yuda kuanzia Dani hadi Beer-Sheba.” Ish-Boshethi hakuthubutu kusema neno jingine kwa Abneri, kwa sababu alimwogopa Abneri. Ndipo Abneri akatuma wajumbe kwa niaba yake kwa Daudi, kumwambia, “Nchi hii ni ya nani? Fanya mapatano na mimi, nami nitakusaidia kuiweka Israeli yote juu yako.” Daudi akasema, “Vyema, nitafanya mapatano nawe. Lakini nahitaji jambo moja kwako: Usije mbele yangu hadi umemleta Mikali binti Sauli wakati utakapokuja kuniona.” Kisha Daudi akapeleka wajumbe kwa Ish-Boshethi mwana wa Sauli, kudai, “Nipe Mikali mke wangu, ambaye nilimposa mwenyewe kwa mahari ya magovi mia moja ya Wafilisti.” Kwa hiyo Ish-Boshethi akatoa amri kwamba Mikali achukuliwe kutoka kwa Paltieli mumewe, mwana wa Laishi. Hata hivyo, mumewe alienda pamoja naye, akilia nyuma ya mkewe njia yote hadi Bahurimu. Ndipo Abneri akamwambia Paltieli, “Rudi nyumbani!” Kwa hiyo akarudi. Abneri akafanya shauri pamoja na wazee wa Israeli, akasema, “Muda mrefu mmetaka kumfanya Daudi mfalme wenu. Sasa fanyeni hivyo! Kwa maana BWANA alimwahidi Daudi akisema, ‘Kupitia Daudi mtumishi wangu nitawaokoa watu wangu Israeli kutoka mikononi mwa Wafilisti na kutoka mikononi mwa adui zako wote.’ ” Pia Abneri mwenyewe akazungumza na kabila la Benyamini. Kisha akaenda Hebroni kumwambia Daudi kila kitu ambacho Israeli na nyumba yote ya Benyamini walichotaka kufanya. Abneri, aliyekuwa na watu ishirini pamoja naye, alipokuja kwa Daudi huko Hebroni, Daudi akamwandalia karamu pamoja na watu wake. Ndipo Abneri akamwambia Daudi, “Niache niende mara moja nikakusanye Israeli yote kwa ajili ya mfalme bwana wangu, ili waweze kufanya mapatano na wewe, ili uweze kutawala yale yote moyo wako unaonea shauku.” Basi Daudi akamuaga Abneri, naye akaenda kwa amani.