2 Samweli 13:23-39
2 Samweli 13:23-39 NENO
Miaka miwili baadaye, wakati wakata manyoya ya kondoo wa Absalomu walipokuwa huko Baal-Hasori karibu na mpaka wa Efraimu, alialika wana wote wa mfalme kuja huko. Absalomu akaenda kwa mfalme na kumwambia, “Mtumishi wako ninao wakata manyoya ya kondoo waliokuja. Tafadhali, je, mfalme na maafisa wake wanaweza kuungana nami?” Mfalme akajibu, “La, mwanangu. Si lazima sote tuje, tutakuwa tu mzigo kwako.” Ingawa Absalomu alimsihi sana, mfalme alikataa kwenda, lakini akambariki. Basi Absalomu akasema, “Kama hutakuja, tafadhali mruhusu ndugu yangu Amnoni twende pamoja naye.” Mfalme akamuuliza, “Kwa nini aende pamoja nawe?” Lakini Absalomu alimsihi, kwa hiyo mfalme akamtuma Amnoni pamoja na wana wengine wa mfalme waliobaki. Absalomu aliagiza watu wake, “Sikilizeni! Amnoni atakapokuwa amekunywa mvinyo na kulewa sana nami nikiwaambia, ‘Mpigeni Amnoni,’ basi muueni. Msiogope. Je, si mimi niliyewapa amri hii? Kuweni hodari na wenye ushujaa.” Kwa hiyo watu wa Absalomu wakamtendea Amnoni kama vile Absalomu alivyokuwa amewaagiza. Ndipo wana wote wa mfalme wakainuka, wakapanda nyumbu zao, wakakimbia. Wakiwa njiani, taarifa ilimjia Daudi, kusema: “Absalomu amewaua wana wote wa mfalme; hakuna hata mmoja aliyesalia.” Mfalme akasimama, akararua nguo zake, akalala chini ardhini; nao watumishi wake wote wakasimama kando yake na nguo zao zikiwa zimeraruliwa. Lakini Yonadabu mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akasema, “Bwana wangu asifikiri kwamba wamewaua wana wote wa mfalme; ni Amnoni peke yake ndiye alikufa. Hili limekuwa kusudi la moyo wa Absalomu tangu siku ile Amnoni alipomtendea jeuri Tamari, dada yake. Mfalme bwana wangu asisumbuliwe na taarifa kwamba wamewaua wana wote wa mfalme. Ni Amnoni peke yake aliyekufa.” Wakati huo, Absalomu akawa amekimbia. Basi mlinzi akaangalia, naye akaona watu wengi barabarani magharibi yake, wakishuka kutoka upande wa kilima. Mlinzi akaenda akamwambia mfalme, “Naona watu wakitokea upande wa Horonaimu, huko upande wa kilimani.” Yonadabu akamwambia mfalme, “Tazama, wana wa mfalme wako hapa; imekuwa kama vile mtumishi wako alivyosema.” Mara alipomaliza kusema, wana wa mfalme wakaingia ndani wakiomboleza kwa makelele. Pia mfalme na watumishi wake wote wakalia sana kwa uchungu. Absalomu akakimbia na kwenda kwa Talmai mwana wa Amihudi, mfalme wa Geshuri. Lakini Mfalme Daudi akaomboleza kwa ajili ya mwanawe kila siku. Baada ya Absalomu kukimbia na kwenda Geshuri, akakaa huko miaka mitatu. Roho ya Mfalme Daudi ikatamani kumwendea Absalomu, kwa maana mfalme alikuwa amefarijika kuhusu kifo cha Amnoni.