2 Petro 3:8-15
2 Petro 3:8-15 NENO
Lakini wapendwa, msisahau neno hili: kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba. Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; navyo vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilicho ndani yake kitaunguzwa. Kwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, je, ninyi imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu, mkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu. Siku hiyo italeta mbingu kuchomwa moto na kutoweka, na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto. Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake. Kwa sababu hii, wapendwa, kwa kuwa mnatazamia mambo haya, fanyeni bidii ili awakute bila mawaa wala dosari, na mkiwa na amani kwake. Hesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile ndugu yetu mpendwa Paulo alivyowaandikia kwa hekima ile aliyopewa na Mungu.