2 Petro 3:1-7
2 Petro 3:1-7 NENO
Wapendwa, huu ndio waraka wangu wa pili ninaowaandikia. Katika nyaraka hizi mbili ninajaribu kuziamsha nia zenu safi kwa mawazo makamilifu. Nataka ninyi mkumbuke maneno yaliyosemwa zamani na manabii watakatifu na ile amri ya Bwana na Mwokozi wetu mliyopewa kupitia kwa mitume wenu. Kwanza kabisa, ni lazima mfahamu kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka, wakidhihaki na kuzifuata tamaa zao mbovu. Watasema, “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake? Tangu baba zetu walipofariki, kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa.” Lakini wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwa tangu zamani, nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa maji. Ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa kwa hayo maji na kuangamizwa. Kwa neno lilo hilo, mbingu za sasa na dunia zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.