Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 21:16-26

2 Wafalme 21:16-26 NENO

Zaidi ya hayo, Manase pia alimwaga damu nyingi isiyo na hatia, hivi kwamba aliijaza Yerusalemu kutoka mwanzo hadi mwisho, mbali na dhambi ambayo alikuwa amesababisha Yuda kufanya, na hivyo wakatenda maovu machoni pa BWANA. Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Manase, na yote aliyoyafanya, pamoja na dhambi alizotenda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Manase akalala na baba zake, akazikwa katika bustani ya jumba lake la kifalme, katika bustani ya Uza. Naye Amoni mwanawe akawa mfalme baada yake. Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka miwili. Mamaye aliitwa Meshulemethi binti Haruzi, kutoka Yotba. Akatenda maovu machoni mwa BWANA, kama baba yake Manase alivyofanya. Akaenenda katika njia zote za baba yake, akaabudu sanamu ambazo baba yake aliziabudu na kuzisujudia. Akamwacha BWANA, Mungu wa baba zake, wala hakuenenda katika njia za BWANA. Watumishi wa Amoni wakampangia njama, nao wakamuua ndani ya jumba lake la kifalme. Kisha watu wa nchi wakawaua wale wote waliokuwa wamepanga njama dhidi ya Mfalme Amoni. Wakamfanya Yosia mwanawe kuwa mfalme mahali pake. Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Amoni na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Akazikwa kwenye kaburi lake katika bustani ya Uza. Naye Yosia mwanawe akawa mfalme baada yake.