2 Wafalme 20:12-21
2 Wafalme 20:12-21 NENO
Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani mfalme wa Babeli, akamtumia Hezekia barua na zawadi, kwa sababu alikuwa amesikia habari za kuugua kwa Hezekia. Hezekia akawapokea wale wajumbe na kuwaonesha vitu vyote vilivyokuwa katika ghala zake: yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha na kila kitu kilichokuwa katika hazina yake. Hapakuwa na kitu katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonesha. Ndipo nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumuuliza, “Watu hao walisema nini, na wametoka wapi?” Hezekia akamjibu, “Wametoka nchi ya mbali. Walikuja kutoka Babeli.” Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?” Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu. Hakuna kitu katika hazina yangu ambacho sikuwaonesha.” Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la BWANA: Hakika wakati unakuja ambapo vitu vyote katika jumba lako, na vyote ambavyo baba zako waliweka akiba hadi siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna chochote kitakachosalia, asema BWANA. Nao baadhi ya wazao wako, mwili wako na damu yako mwenyewe watakaozaliwa kwako, watachukuliwa mateka, nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.” Hezekia akamjibu Isaya, “Neno la BWANA ulilosema ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, “Si patakuwa na amani na usalama wakati wa uhai wangu?” Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Hezekia, mafanikio yake yote, na jinsi alivyotengeneza bwawa na mfereji ulioleta maji katika mji, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Hezekia akalala na baba zake. Naye Manase mwanawe akawa mfalme baada yake.