2 Nyakati 7
7
Hekalu lawekwa wakfu
(1Fal 8:62‑66)
1Baada ya Sulemani kumaliza kuomba, moto ukashuka kutoka mbinguni na kuteketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu, nao utukufu wa Bwana ukalijaza Hekalu. 2Makuhani hawakuweza kuingia ndani ya Hekalu la Bwana kwa sababu utukufu wa Bwana ulilijaza. 3Waisraeli wote walipoona moto ukishuka na utukufu wa Bwana ukiwa juu ya Hekalu, wakapiga magoti sakafuni wakasujudu, nyuso zao zikigusa chini, wakamwabudu na kumshukuru Bwana, wakisema,
“Yeye ni mwema;
fadhili zake zadumu milele.”
4Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za Bwana Mungu. 5Naye Mfalme Sulemani akatoa dhabihu ya ngʼombe elfu ishirini na mbili pamoja na kondoo na mbuzi elfu mia moja na ishirini. Ndivyo mfalme na watu wote walivyoweka wakfu Hekalu la Mungu. 6Makuhani wakasimama kwenye nafasi zao, vivyo hivyo Walawi wakiwa na vyombo vya uimbaji vya Bwana ambavyo Mfalme Daudi alikuwa ametengeneza kwa ajili ya kumsifu Bwana, navyo vilitumika aliposhukuru, akisema, “Fadhili zake zadumu milele.” Mkabala na Walawi, makuhani walipiga tarumbeta zao, nao Waisraeli wote walikuwa wamesimama.
7Sulemani akaweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya Hekalu la Bwana, na hapo akatoa sadaka za kuteketezwa na mafuta ya wanyama wa sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba aliyokuwa ametengeneza haikutosha kuweka sadaka hizo zote za kuteketezwa, sadaka za nafaka, na za mafuta.
8Hivyo Sulemani akaiadhimisha sikukuu wakati ule kwa muda wa siku saba, na Waisraeli wote pamoja naye. Walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka Lebo-Hamathi hadi Kijito cha Misri. 9Katika siku ya nane walifanya kusanyiko, kwa sababu walikuwa wameadhimisha kuwekwa wakfu kwa madhabahu kwa muda wa siku saba, na sikukuu kwa muda wa siku nyingine saba. 10Katika siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa saba Sulemani akawaaga watu waende nyumbani mwao, wakishangilia na kufurahi mioyoni mwao, kwa wema mwingi Bwana Mungu aliomtendea Daudi na Sulemani na kwa ajili ya watu wake Israeli.
Bwana amtokea Sulemani
(1Fal 9:1‑9)
11Sulemani alipomaliza kujenga Hekalu la Bwana na jumba la kifalme, naye akiwa amefanikiwa kutenda yale yote aliyokuwa nayo moyoni mwake kufanya katika Hekalu la Bwana na katika jumba lake mwenyewe la kifalme, 12Bwana akamtokea Sulemani usiku na kumwambia:
“Nimesikia maombi yako nami nimechagua mahali hapa kwa ajili yangu mwenyewe kuwa Hekalu kwa ajili ya dhabihu.
13“Nitakapofunga mbingu ili isiwepo mvua, au nikiamuru nzige kula mazao ya nchi au nikituma tauni miongoni mwa watu wangu, 14ikiwa watu wangu, wanaoitwa kwa Jina langu, watajinyenyekeza na kuomba na kuutafuta uso wangu, na kuacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao, na nitaiponya nchi yao. 15Sasa macho yangu yatafumbuka na masikio yangu yatasikiliza kwa makini maombi yanayoombwa mahali hapa. 16Kwa maana sasa nimechagua na kutakasa Hekalu hili ili Jina langu lipate kuwa humo milele. Macho yangu na moyo wangu vitakuwepo daima.
17“Kwako wewe, ukienenda mbele zangu kama Daudi baba yako alivyoenenda, na kufanya yote ninayokuamuru, nawe ukizishika amri zangu na sheria zangu, 18nitakiimarisha kiti chako cha ufalme kama nilivyoagana na Daudi baba yako niliposema, ‘Hutakosa kamwe mtu wa kutawala Israeli.’
19“Lakini mkigeuka na kuyaacha maagizo na amri nilizowapa na kwenda kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, 20ndipo nitakapoingʼoa Israeli kutoka nchi yangu niliyowapa, nami nitalikataa Hekalu hili nililolitakasa kwa ajili ya Jina langu. Nitalifanya kitu cha kudharauliwa na kitu cha kudhihakiwa miongoni mwa watu wote. 21Ingawa Hekalu hili linavutia sana sasa, wote watakaolipita watashangaa na kusema, ‘Kwa nini Bwana amefanya kitu kama hiki katika nchi hii na kwa Hekalu hili?’ 22Watu watajibu, ‘Ni kwa sababu wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewatoa Misri, nao wamekumbatia miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia, ndiyo sababu ameyaleta maafa haya yote juu yao.’ ”
Iliyochaguliwa sasa
2 Nyakati 7: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.