1 Wafalme 8:1-11
1 Wafalme 8:1-11 NENO
Kisha Mfalme Sulemani akawaita mbele zake huko Yerusalemu wazee wa Israeli, viongozi wote wa makabila na wakuu wa jamaa za Waisraeli, ili walilete Sanduku la Agano la BWANA kutoka Sayuni, Mji wa Daudi. Wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa Mfalme Sulemani wakati wa sikukuu ya mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba. Wazee wote wa Israeli walipofika, makuhani wakajitwika lile Sanduku, nao wakalipandisha Sanduku la BWANA, na Hema la Kukutania, pamoja na vyombo vyote vitakatifu vilivyokuwa ndani yake. Makuhani na Walawi wakavibeba, naye Mfalme Sulemani na kusanyiko lote la Israeli waliokuwa wamemzunguka wakasimama mbele ya hilo Sanduku, nao wakatoa dhabihu za kondoo na ngʼombe nyingi kiasi kwamba idadi yao haikuweza kuandikwa au kuhesabika. Makuhani wakalileta Sanduku la Agano la BWANA hadi mahali pake ndani ya mahali patakatifu sana humo Hekaluni, ndipo Patakatifu pa Patakatifu, na kuliweka chini ya mabawa ya makerubi. Makerubi yalitandaza mabawa yao juu ya mahali pa Sanduku la Agano na kutia kivuli Sanduku pamoja na mipiko yake ya kubebea. Mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana kiasi kwamba ncha zake zilionekana kutoka Mahali Patakatifu mbele ya Patakatifu pa Patakatifu, lakini sio nje ya Mahali Patakatifu. Hiyo mipiko ipo hata leo. Ndani ya Sanduku hapakuwa na kitu kingine isipokuwa vile vibao viwili vya mawe ambavyo Musa aliviweka ndani yake huko Horebu, mahali BWANA alipofanya agano na Waisraeli baada ya kutoka Misri. Makuhani walipoondoka katika Mahali Patakatifu, wingu likajaza Hekalu la BWANA. Nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa BWANA ulijaza Hekalu lake.