1 Wafalme 13:1-10
1 Wafalme 13:1-10 NENO
Kwa neno la BWANA, mtu wa Mungu alifika Betheli kutoka Yuda wakati Yeroboamu alipokuwa amesimama kando ya madhabahu ili kutoa sadaka. Akapiga kelele dhidi ya madhabahu kwa neno la BWANA: “Ee madhabahu, ee madhabahu! Hivi ndivyo asemavyo BWANA: ‘Mwana aitwaye Yosia atazaliwa katika nyumba ya Daudi. Juu yako atawatoa dhabihu makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia ambao hutoa sadaka hapa, nayo mifupa ya wanadamu itateketezwa juu yako.’ ” Siku hiyo hiyo, mtu wa Mungu akatoa ishara: “Hii ndiyo ishara BWANA aliyotangaza: Madhabahu haya yatapasuka na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.” Mfalme Yeroboamu aliposikia kile mtu wa Mungu alichosema, alipopiga kelele dhidi ya madhabahu huko Betheli, akanyoosha mkono wake kutoka madhabahuni na kusema, “Mkamateni!” Lakini mkono aliounyoosha kumwelekea yule mtu ukakauka kiasi kwamba hakuweza kuurudisha. Pia, madhabahu yakapasuka na majivu yakamwagika, sawasawa na ishara iliyotolewa na mtu wa Mungu kwa neno la BWANA. Kisha mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “Niombee kwa BWANA Mungu wako ili mkono wangu upate kupona.” Kwa hiyo mtu wa Mungu akamwombea kwa BWANA, nao mkono wa mfalme ukapona na kurudi ulivyokuwa hapo awali. Mfalme akamwambia yule mtu wa Mungu, “Twende nyumbani mwangu upate chakula, nami nitakupa zawadi.” Lakini yule mtu wa Mungu akamjibu mfalme, “Hata kama ungenipa nusu ya mali yako, nisingeenda pamoja nawe, wala nisingekula mkate au kunywa maji hapa. Kwa kuwa niliagizwa kwa neno la BWANA: ‘Kamwe usile mkate wala usinywe maji au kurudi kwa njia uliyojia.’ ” Hivyo, akafuata njia nyingine na hakurudi kupitia njia aliyokuwa ameijia Betheli.