Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Nyakati 29:10-25

1 Nyakati 29:10-25 NEN

Daudi akamhimidi BWANA mbele ya kusanyiko lote, akisema: “Uhimidiwe wewe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, tangu milele hata milele. Ukuu na uweza, ni vyako, Ee BWANA, na utukufu na enzi na uzuri, kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani ni chako wewe. Ee BWANA, ufalme ni wako; umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote. Utajiri na heshima vyatoka kwako; wewe ndiwe utawalaye vitu vyote. Mikononi mwako kuna nguvu na uweza ili kuinua na kuwapa wote nguvu, Sasa, Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu Jina lako tukufu. “Lakini mimi ni nani, nao watu wangu ni nani, hata tuweze kukutolea kwa ukarimu namna hii? Vitu vyote vyatoka kwako, nasi tumekutolea tu vile vitokavyo mkononi mwako. Sisi ni wageni na wapitaji machoni pako, kama walivyokuwa baba zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli, bila tumaini. Ee BWANA Mungu wetu, kwa wingi wote huu ambao tumekutolea kwa kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina lako Takatifu, vimetoka mkononi mwako, navyo vyote ni mali yako. Ninajua, Mungu wangu, kwamba wewe huujaribu moyo na unapendezwa na unyofu. Vitu hivi vyote nimetoa kwa hiari na kwa moyo mnyofu. Nami sasa nimeona kwa furaha jinsi watu wako walioko hapa kwa hiari yao walivyokutolea wewe. Ee BWANA, Mungu wa baba zetu Abrahamu, Isaki na Israeli, weka shauku hii ndani ya mioyo ya watu wako daima na uifanye mioyo yao iwe na uaminifu kwako. Nawe umpe mwanangu Solomoni kujitolea kwako kwa moyo wote ili kuzishika amri zako, masharti yako, maagizo yako na kufanya kila kitu ili kujenga Hekalu hili la fahari ambalo kwa ajili yake nimetoa.” Ndipo Daudi akaliambia kusanyiko lote, “Mhimidini BWANA Mungu wenu.” Hivyo wote wakamhimidi BWANA, Mungu wa baba zao. Wakasujudu na kuanguka kifudifudi mbele za BWANA na mfalme. Siku ya pili yake wakamtolea BWANA dhabihu na sadaka za kuteketezwa: mafahali 1,000, kondoo dume 1,000 na wana-kondoo dume 1,000, pamoja na sadaka za kinywaji na sadaka nyingine nyingi sana kwa ajili ya Israeli. Wakala na kunywa kwa furaha kubwa mbele za BWANA siku ile. Wakamtawaza Solomoni mwana wa Daudi mara ya pili kuwa mfalme, wakamtia mafuta kwa ajili ya BWANA ili awe mfalme na Sadoki kuwa kuhani. Solomoni akaketi kwenye kiti cha enzi cha BWANA kuwa mfalme mahali pa Daudi baba yake. Akafanikiwa sana na Israeli wote wakamtii. Maafisa wote na mashujaa, pamoja na wana wote wa Daudi, wakaahidi kumtii Mfalme Solomoni. BWANA akamtukuza sana Solomoni mbele ya Israeli wote na kumvika fahari ya kifalme ambayo hakuna mfalme yeyote wa Israeli kabla yake aliwahi kuwa nayo.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha