Mwanzo 46
46
Yakobo aenda Misri
1Hivyo Israeli akaondoka na mali yake yote. Alipofika Beer-Sheba, akamtolea dhabihu Mungu wa Isaka baba yake.
2 Mungu akanena na Israeli katika maono usiku na kusema, “Yakobo! Yakobo!”
Akamjibu, “Mimi hapa.”
3 Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako. Usiogope kushuka Misri, kwa maana huko nitakufanya taifa kubwa. 4Nitashuka Misri pamoja nawe, nami hakika nitakurudisha tena Kanaani. Mikono ya Yusufu mwenyewe ndiyo itakayofunga macho yako.”
5 Ndipo Yakobo akaondoka Beer-Sheba, nao wana wa Israeli wakamchukua baba yao Yakobo, na watoto wao na wake zao katika magari ya kukokotwa yale Farao alikuwa amempelekea kumsafirisha. 6Wakachukua pia mifugo yao na mali walizokuwa wamezipata Kanaani; Yakobo na uzao wake wote wakashuka Misri. 7Akawachukua wanawe na binti zake, wajukuu wake wa kiume na wa kike, yaani uzao wake wote hadi Misri.
8Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli (Yakobo na wazao wake), walioenda Misri:
Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo.
9Wana wa Reubeni ni:
Hanoki, Palu, Hesroni, na Karmi.
10 Wana wa Simeoni ni:
Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari, na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani.
11Wana wa Lawi ni:
Gershoni, Kohathi, na Merari.
12 Wana wa Yuda ni:
Eri, Onani, Shela, Peresi, na Zera (lakini Eri na Onani walifariki katika nchi ya Kanaani).
Wana wa Peresi ni:
Hesroni na Hamuli.
13Wana wa Isakari ni:
Tola, Puva, Yashubu, na Shimroni.
14 Wana wa Zabuloni ni:
Seredi, Eloni, na Yaleeli.
15 Hawa ndio wana wa Lea aliomzalia Yakobo huko Padan-Aramu, pamoja na binti yake Dina. Jumla ya hawa wanawe wa kiume na wa kike walikuwa thelathini na watatu.
16 Wana wa Gadi ni:
Sefoni, Hagi, Shuni, Esboni, Eri, Arodi, na Areli.
17 Wana wa Asheri ni:
Imna, Ishva, Ishvi, na Beria. Dada yao alikuwa Sera.
Wana wa Beria ni:
Heberi na Malkieli.
18Hawa ndio watoto Zilpa aliomzalia Yakobo, ambaye Labani alimpa binti yake Lea; jumla yao walikuwa kumi na sita.
19Wana wa Raheli mke wa Yakobo ni:
Yusufu na Benyamini.
20 Huko Misri, Asenathi binti Potifera, aliyekuwa kuhani wa mji wa Oni#46:20 yaani Heliopoli (Mji wa jua), alimzalia Yusufu wana wawili: Manase na Efraimu.
21 Wana wa Benyamini ni:
Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu, na Ardi.
22Hawa ndio wana wa Raheli aliomzalia Yakobo; jumla yao ni kumi na wanne.
23Mwana wa Dani ni:
Hushimu.
24 Wana wa Naftali ni:
Yaseeli, Guni, Yeseri, na Shilemu.
25 Hawa walikuwa wana wa Bilha aliomzalia Yakobo, ambaye Labani alikuwa amempa Raheli binti yake; jumla yao walikuwa saba.
26 Wote walioenda Misri pamoja na Yakobo, waliokuwa wazao wake hasa pasipo kuhesabu wakwe wake, walikuwa watu sitini na sita. 27Pamoja na wana wawili waliozaliwa na Yusufu huko Misri, jumla ya jamaa ya Yakobo walioenda Misri walikuwa sabini.
28 Basi Yakobo akamtanguliza Yuda aende kwa Yusufu ili amwelekeze njia ya Gosheni. Walipofika nchi ya Gosheni, 29Yusufu aliandaa gari lake la vita, na akaenda Gosheni kumlaki baba yake, Israeli. Mara Yusufu alipofika mbele yake, alimkumbatia baba yake, akalia kwa muda mrefu.
30 Israeli akamwambia Yusufu, “Sasa niko tayari kufa, kwa kuwa nimejionea mwenyewe kwamba bado uko hai.”
31 Ndipo Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, “Nitapanda kwa Farao na kumwambia, ‘Ndugu zangu na watu wa nyumbani mwa baba yangu, walioishi katika nchi ya Kanaani, wamekuja kwangu. 32Watu hao ni wafugaji; wao huchunga mifugo, na wamekuja na makundi ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, pamoja na kila kitu walicho nacho.’ 33Farao atakapowaita na kuwauliza, ‘Kazi yenu ni nini?’ 34mjibuni, ‘Watumishi wako wamekuwa wafugaji wa wanyama tangu ujana wetu hadi sasa, kama baba zetu walivyokuwa.’ Ndipo mtaruhusiwa kukaa katika nchi ya Gosheni, kwa kuwa wafugaji wote ni chukizo kwa Wamisri.”
Právě zvoleno:
Mwanzo 46: NEN
Zvýraznění
Kopírovat
Porovnat
Sdílet
Chceš mít své zvýrazněné verše uložené na všech zařízeních? Zaregistruj se nebo se přihlas
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.