Tafuta matokeo ya: 1 Samuel 15
1 Sam 15:1 (SUV)
Wakati huo Samweli akamwambia Sauli, BWANA alinipeleka nikutie mafuta, uwe mfalme wa watu wake Israeli; basi sasa, isikilize sauti na maneno ya BWANA.
1 Sam 15:2 (SUV)
BWANA wa majeshi asema hivi, Nimeyatia moyoni mwangu mambo hayo Amaleki waliyowatenda Israeli, jinsi walivyowapinga njiani, hapo walipopanda kutoka Misri.
1 Sam 15:3 (SUV)
Basi sasa enda ukawapige Amaleki, na kuviharibu kabisa vitu vyote walivyo navyo, wala msiwaachilie; bali waueni, mwanamume na mwanamke, mtoto naye anyonyaye, ng’ombe na kondoo, ngamia na punda.
1 Sam 15:4 (SUV)
Ndipo Sauli akawaita watu, akawahesabu huko Telemu, askari waliopanda farasi mia mbili elfu, na watu wa Yuda kumi elfu.
1 Sam 15:5 (SUV)
Sauli akaufikilia mji wa Amaleki, akauvizia bondeni.
1 Sam 15:6 (SUV)
Sauli akawaambia Wakeni, Haya! Enendeni zenu, mkashuke ili kujitenga na Waamaleki, nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao; maana mliwatendea wana wa Israeli mema, walipopanda kutoka Misri. Basi hao Wakeni wakaondoka, wakajitenga na Waamaleki.
1 Sam 15:7 (SUV)
Sauli akawapiga Waamaleki, toka Havila uendapo Shuri, unaokabili Misri.
1 Sam 15:8 (SUV)
Akamkamata Agagi, mfalme wa Waamaleki, yu hai, akawaangamiza hao watu wote kwa upanga.
1 Sam 15:9 (SUV)
Lakini Sauli na watu wake wakamwacha Agagi hai, na katika kondoo walio wazuri, na ng’ombe, na vinono, na wana-kondoo, na cho chote kilicho chema, wala hawakukubali kuwaangamiza; bali cho chote kilichokuwa kibaya na kibovu, ndicho walichokiangamiza kabisa.
1 Sam 15:10 (SUV)
Ndipo neno la BWANA likamjia Samweli, kusema,
1 Sam 15:11 (SUV)
Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia BWANA usiku kucha.
1 Sam 15:12 (SUV)
Samweli akaondoka asubuhi na mapema ili aonane na Sauli; Samweli akaambiwa ya kwamba, Sauli alifika Karmeli, na tazama, akajisimamishia ukumbusho, akageuka, akapita, akatelemkia Gilgali.
1 Sam 15:13 (SUV)
Samweli akamwendea Sauli; naye Sauli akamwambia, Ubarikiwe na BWANA, nimeitimiza amri ya BWANA.
1 Sam 15:14 (SUV)
Samweli akasema, Maana yake nini, basi, hiki kilio cha kondoo masikioni mwangu, na huu mlio wa ng’ombe ninaousikia?
1 Sam 15:15 (SUV)
Sauli akasema, Wamewaleta kutoka kwa Waamaleki; maana watu waliwaacha hai kondoo na ng’ombe walio wazuri, ili wawatoe dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, nao waliosalia tumewaangamiza kabisa.
1 Sam 15:16 (SUV)
Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Ngoja, nami nitakuambia neno aliloniambia BWANA usiku huu. Naye akamwambia, Haya, sema.
1 Sam 15:17 (SUV)
Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye BWANA akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli.
1 Sam 15:18 (SUV)
Kisha BWANA akakutuma safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata watakapoangamia.
1 Sam 15:19 (SUV)
Mbona, basi, hukuitii sauti ya BWANA, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA?
1 Sam 15:20 (SUV)
Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya BWANA, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa.
1 Sam 15:21 (SUV)
Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng’ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, huko Gilgali.
1 Sam 15:22 (SUV)
Naye Samweli akasema, je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.
1 Sam 15:23 (SUV)
Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.
1 Sam 15:24 (SUV)
Ndipo Sauli akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya BWANA, pia na maneno yako; kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao.
1 Sam 15:25 (SUV)
Basi sasa, nakuomba, unisamehe dhambi yangu; rudi pamoja nami, nipate kumwabudu BWANA.