Tafuta matokeo ya: Mathayo 6:33
Mathayo 2:22 (BHN)
Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao, mwanawe Herode, alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye, baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda pande za Galilaya,
Mathayo 2:23 (BHN)
akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii: “Ataitwa Mnazare.”
Mathayo 3:1 (BHN)
Siku zile Yohane Mbatizaji alitokea, akaanza kuhubiri katika jangwa la Yudea:
Mathayo 3:2 (BHN)
“Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”
Mathayo 5:11 (BHN)
“Heri yenu nyinyi watu wakiwatukana, wakiwadhulumu na kuwasingizia kila aina ya uovu kwa ajili yangu.
Mathayo 5:12 (BHN)
Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Hivyo ndivyo walivyowadhulumu manabii waliokuwako kabla yenu.
Mathayo 5:13 (BHN)
“Nyinyi ni chumvi ya dunia. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake itakolezwa na nini? Haifai kitu tena, ila hutupwa nje na kukanyagwa na watu.
Mathayo 5:14 (BHN)
“Nyinyi ni mwanga wa ulimwengu! Mji uliojengwa juu ya mlima hauwezi kufichika.
Mathayo 5:15 (BHN)
Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa debe, ila huiweka juu ya kinara ili iwaangazie wote waliomo nyumbani.
Mathayo 5:17 (BHN)
“Msidhani kuwa nimekuja kutangua sheria na mafundisho ya manabii. Sikuja kutangua bali kukamilisha.
Mathayo 5:18 (BHN)
Kweli nawaambieni, mpaka hapo mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata nukta moja au sehemu ndogo kabisa ya sheria itakayoondolewa, mpaka yote yametimia.
Mathayo 5:19 (BHN)
Basi, yeyote atakayevunja hata amri moja ndogo kuliko zote, na kuwafundisha wengine wafanye hivyo, huyo atakuwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni. Lakini yule atakayezishika na kuwafundisha wengine, huyo atakuwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.
Mathayo 5:20 (BHN)
Ndio maana nawaambieni, wema wenu usipozidi ule wa waalimu wa sheria na wa Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
Mathayo 5:21 (BHN)
“Mmekwisha sikia ya kuwa watu wa kale waliambiwa: ‘Usiue! Atakayeua lazima ahukumiwe.’
Mathayo 5:22 (BHN)
Lakini mimi nawaambieni, yeyote anayemkasirikia ndugu yake, lazima ahukumiwe. Anayemdharau ndugu yake atapelekwa mahakamani. Anayemwita ndugu yake: ‘Pumbavu’ atastahili kuingia katika moto wa Jehanamu.
Mathayo 5:23 (BHN)
“Basi, ukipeleka sadaka yako mbele ya madhabahu na hapo ukakumbuka kwamba ndugu yako ana ugomvi nawe,
Mathayo 5:24 (BHN)
iache sadaka yako mbele ya madhabahu, nenda kwanza ukapatane na ndugu yako, ndipo urudi utoe sadaka yako.
Mathayo 5:25 (BHN)
“Patana na mshtaki wako upesi mkiwa bado njiani kwenda mahakamani. La sivyo, mshtaki wako atakukabidhi kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa askari, nawe utafungwa gerezani.
Mathayo 5:26 (BHN)
Kweli nakuambia, hutatoka humo mpaka umelipa senti ya mwisho.
Mathayo 5:27 (BHN)
“Mmesikia kwamba watu waliambiwa: ‘Usizini!’
Mathayo 5:28 (BHN)
Lakini mimi nawaambieni, atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani, amekwisha zini naye moyoni mwake.
Mathayo 5:29 (BHN)
Basi, kama jicho lako la kulia linakukosesha, lingoe ukalitupe mbali. Afadhali zaidi kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote kutupwa katika moto wa Jehanamu.
Mathayo 5:30 (BHN)
Na kama mkono wako wa kulia unakukosesha, ukate ukautupe mbali. Afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote uende katika moto wa Jehanamu.
Mathayo 5:31 (BHN)
“Ilikwisha semwa pia: ‘Anayemwacha mke wake, yampasa ampe hati ya talaka’.
Mathayo 5:32 (BHN)
Lakini mimi nawaambieni, anayempa mkewe talaka, isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, anamfanya azini; na mwanamume akimwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini.