Sefania 3:8-13
Sefania 3:8-13 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kwa hiyo ningojeni mimi Mwenyezi-Mungu, ngoja siku nitakapoinuka kutoa mashtaka. Nimeamua kuyakusanya mataifa na falme, kuyamwagia ghadhabu yangu, kadhalika na ukali wa hasira yangu. Dunia yote itateketezwa kwa moto wa ghadhabu yangu. “Wakati huo nitaibadili lugha ya watu, nitawawezesha kusema lugha adili ili waniite mimi Mwenyezi-Mungu, na kuniabudu kwa moyo mmoja. Kutoka ng'ambo ya mito ya Kushi watu wangu wanaoniomba ambao wametawanyika, wataniletea sadaka yangu. “Siku hiyo, haitakulazimu kuona aibu, kutokana na matendo yako ya kuniasi, maana nitawaondoa miongoni mwako wale wanaojigamba na kujitukuza nawe hutakuwa na kiburi tena katika mlima wangu mtakatifu. Nitakuachia watu wapole na wanyenyekevu ambao watakimbilia usalama kwangu mimi Mwenyezi-Mungu. Waisraeli watakaobaki, hawatatenda mabaya wala hawatasema uongo; wala kwao hatapatikana mdanganyifu yeyote. Watapata malisho na kulala wala hakuna mtu atakayewatisha.”
Sefania 3:8-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi ningojeeni, asema BWANA, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu; kwa maana dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wangu. Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la BWANA, wamtumikie kwa nia moja. Maana toka nchi iliyo mbali na mito ya Kushi, waniombao dua, yaani, binti za watu wangu waliotawanyika, wataleta matoleo yangu. Siku ile hutaaibishwa kwa matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaojigamba na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu. Lakini nitabakiza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la BWANA. Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautakuwa kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewatisha.
Sefania 3:8-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi ningojeni, asema BWANA, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu; kwa maana dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wangu. Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la BWANA, wamtumikie kwa nia moja. Maana toka nchi iliyo mbali na mito ya Kushi, waniombao dua, yaani, binti za watu wangu waliotawanyika, wataleta matoleo yangu. Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu. Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la BWANA. Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya.
Sefania 3:8-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA anasema, “Kwa hiyo ningojee mimi, siku nitakayosimama kuteka nyara. Nimeamua kukusanya mataifa, kukusanya falme na kumimina ghadhabu yangu juu yao, hasira yangu kali yote. Dunia yote itateketezwa kwa moto wa hasira yangu yenye wivu. “Ndipo nitatakasa midomo ya mataifa, kwamba wote waweze kuliitia jina la BWANA na kumtumikia kwa pamoja. Kutoka ngʼambo ya mito ya Kushi watu wangu wanaoniabudu, watu wangu waliotawanyika, wataniletea sadaka. Siku hiyo hutaaibishwa kwa ajili ya makosa yote uliyonitendea, kwa sababu nitawaondoa kutoka mji huu wale wote wanaoshangilia katika kiburi chao. Kamwe hutajivuna tena katika kilima changu kitakatifu. Lakini nitakuachia ndani yako wapole na wanyenyekevu, ambao wanatumaini jina la BWANA. Mabaki ya Israeli hayatafanya kosa; hawatasema uongo, wala udanganyifu hautakuwa katika vinywa vyao. Watakula na kulala wala hakuna yeyote atakayewaogopesha.”