Sefania 3:1-8
Sefania 3:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Ole wake mji wa Yerusalemu, mji mchafu, najisi na mdhalimu. Hausikilizi onyo lolote, wala haukubali kukosolewa. Haukumtegemea Mwenyezi-Mungu kamwe, wala kumkaribia Mungu wake. Viongozi wake ni simba wangurumao, mahakimu wake ni mbwamwitu wenye njaa jioni wasioacha chochote mpaka asubuhi. Manabii wake ni watu wasiojali na wadanganyifu. Makuhani wake wamevitia unajisi vitu vitakatifu na kuihalifu sheria kwa nguvu. Lakini Mwenyezi-Mungu aliye mjini humo ni mwadilifu, yeye hatendi jambo lolote baya. Kila siku asubuhi hudhihirisha kauli yake, naam, kila kunapopambazuka huitekeleza. Lakini wahalifu hawana aibu hata kidogo. Mwenyezi-Mungu asema: “Nimeyafutilia mbali mataifa; kuta zao za kujikinga ni magofu. Barabara zao nimeziharibu, na hamna apitaye humo. Miji yao imekuwa mitupu, bila watu, na bila wakazi. Nilisema, ‘Hakika mji huu watanicha na kukubali kukosolewa; hautaacha kukumbuka mara hizo zote nilizowaadhibu.’ Lakini watu wake walizidisha tamaa zao za kufanya matendo yao kuwa upotovu. “Kwa hiyo ningojeni mimi Mwenyezi-Mungu, ngoja siku nitakapoinuka kutoa mashtaka. Nimeamua kuyakusanya mataifa na falme, kuyamwagia ghadhabu yangu, kadhalika na ukali wa hasira yangu. Dunia yote itateketezwa kwa moto wa ghadhabu yangu.
Sefania 3:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ole wake yeye aliyeasi na kutiwa unajisi, mji wa udhalimu! Hakuitii sauti; hakukubali kurudiwa; hakumwamini BWANA; hakumkaribia Mungu wake. Wakuu wake walio ndani yake ni simba wangurumao; mahakimu wake ni mbwamwitu wa jioni; wasiobakiza kitu chochote mpaka asubuhi. Manabii wake ni watu hafifu, wadanganyifu; makuhani wake wamepatia unajisi patakatifu, wameifanyia sheria udhalimu. BWANA kati yake ni mwenye haki; hatatenda uovu; kila asubuhi hudhihirisha hukumu yake, wala hakomi; bali mtu asiye haki hajui kuona haya. Nimekatilia mbali mataifa, minara yao ina ukiwa; nimeziharibu njia kuu zao, hata hapana mmoja apitaye; miji yao imeangamizwa; hamna mtu hata mmoja, wala hapana akaaye huko. Nilisema, Hakika utaniogopa, utakubali kurudiwa; ili yasikatiliwe mbali makao yake, sawasawa ya yote niliyoagiza katika habari zake; lakini waliondoka mapema na kuyaharibu matendo yao yote. Basi ningojeeni, asema BWANA, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu; kwa maana dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wangu.
Sefania 3:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ole wake yeye aliyeasi na kutiwa unajisi, mji wa udhalimu! Hakuitii sauti; hakukubali kurudiwa; hakumwamini BWANA; hakumkaribia Mungu wake. Wakuu wake walio ndani yake ni simba wangurumao; makadhi wake ni mbwa-mwitu wa jioni; hawasazi kitu cho chote hata siku ya pili. Manabii wake ni watu hafifu, wadanganyifu; makuhani wake wamepatia unajisi patakatifu, wameifanyia sheria udhalimu. BWANA kati yake ni mwenye haki; hatatenda uovu; kila asubuhi hudhihirisha hukumu yake, wala hakomi; bali mtu asiye haki hajui kuona haya. Nimekatilia mbali mataifa, buruji zao zina ukiwa; nimeziharibu njia kuu zao, hata hapana mmoja apitaye; miji yao imeangamizwa; hamna mtu hata mmoja, wala hapana akaaye huko. Nalisema, Hakika utaniogopa, utakubali kurudiwa; ili yasikatiliwe mbali makao yake, sawasawa ya yote niliyoagiza katika habari zake; lakini waliondoka mapema na kuyaharibu matendo yao yote. Basi ningojeni, asema BWANA, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu; kwa maana dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wangu.
Sefania 3:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ole mji wa wadhalimu, waasi na waliotiwa unajisi! Hautii mtu yeyote, haukubali maonyo. Haumtumaini BWANA, haukaribii karibu na Mungu wake. Maafisa wake ni simba wanaonguruma, watawala wake ni mbwa-mwitu wa jioni, ambao hawabakizi chochote kwa ajili ya asubuhi. Manabii wake ni wenye kiburi, ni wadanganyifu. Makuhani wake hunajisi patakatifu na kuihalifu sheria. BWANA aliye ndani yake ni mwenye haki, hafanyi kosa. Asubuhi kwa asubuhi hutoa haki yake, kila kukipambazuka huitimiza, bali mtu dhalimu hana aibu. “Nimeyaangamiza mataifa, ngome zao zimebomolewa. Nimeziacha barabara ukiwa, hakuna anayepita humo. Miji yao imeharibiwa; hakuna mmoja atakayeachwa: hakuna hata mmoja. Niliuambia huo mji, ‘Hakika utaniogopa na kukubali maonyo!’ Ndipo makao yake hayatafutiliwa mbali, wala adhabu zangu zote hazitakuja juu yake. Lakini walikuwa bado na shauku kutenda kwa upotovu katika yote waliyofanya.” BWANA anasema, “Kwa hiyo ningojee mimi, siku nitakayosimama kuteka nyara. Nimeamua kukusanya mataifa, kukusanya falme na kumimina ghadhabu yangu juu yao, hasira yangu kali yote. Dunia yote itateketezwa kwa moto wa hasira yangu yenye wivu.