Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Sefania 3:1-20

Sefania 3:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)

Ole wake mji wa Yerusalemu, mji mchafu, najisi na mdhalimu. Hausikilizi onyo lolote, wala haukubali kukosolewa. Haukumtegemea Mwenyezi-Mungu kamwe, wala kumkaribia Mungu wake. Viongozi wake ni simba wangurumao, mahakimu wake ni mbwamwitu wenye njaa jioni wasioacha chochote mpaka asubuhi. Manabii wake ni watu wasiojali na wadanganyifu. Makuhani wake wamevitia unajisi vitu vitakatifu na kuihalifu sheria kwa nguvu. Lakini Mwenyezi-Mungu aliye mjini humo ni mwadilifu, yeye hatendi jambo lolote baya. Kila siku asubuhi hudhihirisha kauli yake, naam, kila kunapopambazuka huitekeleza. Lakini wahalifu hawana aibu hata kidogo. Mwenyezi-Mungu asema: “Nimeyafutilia mbali mataifa; kuta zao za kujikinga ni magofu. Barabara zao nimeziharibu, na hamna apitaye humo. Miji yao imekuwa mitupu, bila watu, na bila wakazi. Nilisema, ‘Hakika mji huu watanicha na kukubali kukosolewa; hautaacha kukumbuka mara hizo zote nilizowaadhibu.’ Lakini watu wake walizidisha tamaa zao za kufanya matendo yao kuwa upotovu. “Kwa hiyo ningojeni mimi Mwenyezi-Mungu, ngoja siku nitakapoinuka kutoa mashtaka. Nimeamua kuyakusanya mataifa na falme, kuyamwagia ghadhabu yangu, kadhalika na ukali wa hasira yangu. Dunia yote itateketezwa kwa moto wa ghadhabu yangu. “Wakati huo nitaibadili lugha ya watu, nitawawezesha kusema lugha adili ili waniite mimi Mwenyezi-Mungu, na kuniabudu kwa moyo mmoja. Kutoka ng'ambo ya mito ya Kushi watu wangu wanaoniomba ambao wametawanyika, wataniletea sadaka yangu. “Siku hiyo, haitakulazimu kuona aibu, kutokana na matendo yako ya kuniasi, maana nitawaondoa miongoni mwako wale wanaojigamba na kujitukuza nawe hutakuwa na kiburi tena katika mlima wangu mtakatifu. Nitakuachia watu wapole na wanyenyekevu ambao watakimbilia usalama kwangu mimi Mwenyezi-Mungu. Waisraeli watakaobaki, hawatatenda mabaya wala hawatasema uongo; wala kwao hatapatikana mdanganyifu yeyote. Watapata malisho na kulala wala hakuna mtu atakayewatisha.” Imba kwa sauti, ewe Siyoni, paza sauti ee Israeli. Furahi na kushangilia kwa moyo wote, ewe Yerusalemu! Mwenyezi-Mungu amekuondolea hukumu iliyokukabili, amewageuzia mbali adui zako. Mwenyezi-Mungu, mfalme wa Israeli yuko pamoja nawe hutaogopa tena maafa. Siku hiyo, mji wa Yerusalemu utaambiwa: “Usiogope, ee Siyoni, usilegee mikono. Mwenyezi-Mungu, Mungu wako yu pamoja nawe yeye ni shujaa anayekuletea ushindi. Yeye atakufurahia kwa furaha kuu, kwa upendo wake atakujalia uhai mpya. Atakufurahia kwa wimbo wa sauti kubwa, kama vile katika siku ya sikukuu.” Mwenyezi-Mungu asema: “Nitakuondolea maafa yako, nawe hutahitaji kuona aibu kwa ajili yake. Wakati huo, nitawaadhibu wote wanaokukandamiza. Nitawaokoa vilema na kuwakusanya waliotupwa, na kubadili aibu yao kuwa sifa na fahari duniani kote. Wakati huo nitawakusanya, na kuwafanya mjulikane na kusifiwa, miongoni mwa watu wote duniani nitakapowarudishia hali yenu njema nanyi muone kwa macho yenu wenyewe. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Shirikisha
Soma Sefania 3

Sefania 3:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ole wake yeye aliyeasi na kutiwa unajisi, mji wa udhalimu! Hakuitii sauti; hakukubali kurudiwa; hakumwamini BWANA; hakumkaribia Mungu wake. Wakuu wake walio ndani yake ni simba wangurumao; mahakimu wake ni mbwamwitu wa jioni; wasiobakiza kitu chochote mpaka asubuhi. Manabii wake ni watu hafifu, wadanganyifu; makuhani wake wamepatia unajisi patakatifu, wameifanyia sheria udhalimu. BWANA kati yake ni mwenye haki; hatatenda uovu; kila asubuhi hudhihirisha hukumu yake, wala hakomi; bali mtu asiye haki hajui kuona haya. Nimekatilia mbali mataifa, minara yao ina ukiwa; nimeziharibu njia kuu zao, hata hapana mmoja apitaye; miji yao imeangamizwa; hamna mtu hata mmoja, wala hapana akaaye huko. Nilisema, Hakika utaniogopa, utakubali kurudiwa; ili yasikatiliwe mbali makao yake, sawasawa ya yote niliyoagiza katika habari zake; lakini waliondoka mapema na kuyaharibu matendo yao yote. Basi ningojeeni, asema BWANA, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu; kwa maana dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wangu. Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la BWANA, wamtumikie kwa nia moja. Maana toka nchi iliyo mbali na mito ya Kushi, waniombao dua, yaani, binti za watu wangu waliotawanyika, wataleta matoleo yangu. Siku ile hutaaibishwa kwa matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaojigamba na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu. Lakini nitabakiza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la BWANA. Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautakuwa kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewatisha. Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli; Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu. BWANA ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye BWANA, yuko katikati yako; Hutaogopa uovu tena. Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee. BWANA, Mungu wako, yuko katikati yako shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza katika upendo wake, Atakufurahia kwa kuimba. Nitawakusanya wanaousikitikia mkutano wa ibada, hao waliokuwa wa kwako; ambao mzigo uliokuwa juu yake ulikuwa fedheha kwao. Tazama, wakati huo nitawapatiliza watu wote wanaokutesa; nami nitamponya yeye achechemeaye, nami nitamkusanya yeye aliyefukuzwa; nami nitawafanya msifiwe na kujulikana, hao ambao aibu yao ilikuwa katika dunia yote. Wakati huo nitawaingizeni, na wakati huo nitawakusanya; kwa maana nitawafanya ninyi msifiwe na mjulikane, miongoni mwa watu wote wa dunia, nitakapowarudisha wafungwa wenu mbele ya macho yenu, asema BWANA.

Shirikisha
Soma Sefania 3

Sefania 3:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ole wake yeye aliyeasi na kutiwa unajisi, mji wa udhalimu! Hakuitii sauti; hakukubali kurudiwa; hakumwamini BWANA; hakumkaribia Mungu wake. Wakuu wake walio ndani yake ni simba wangurumao; makadhi wake ni mbwa-mwitu wa jioni; hawasazi kitu cho chote hata siku ya pili. Manabii wake ni watu hafifu, wadanganyifu; makuhani wake wamepatia unajisi patakatifu, wameifanyia sheria udhalimu. BWANA kati yake ni mwenye haki; hatatenda uovu; kila asubuhi hudhihirisha hukumu yake, wala hakomi; bali mtu asiye haki hajui kuona haya. Nimekatilia mbali mataifa, buruji zao zina ukiwa; nimeziharibu njia kuu zao, hata hapana mmoja apitaye; miji yao imeangamizwa; hamna mtu hata mmoja, wala hapana akaaye huko. Nalisema, Hakika utaniogopa, utakubali kurudiwa; ili yasikatiliwe mbali makao yake, sawasawa ya yote niliyoagiza katika habari zake; lakini waliondoka mapema na kuyaharibu matendo yao yote. Basi ningojeni, asema BWANA, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu; kwa maana dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wangu. Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la BWANA, wamtumikie kwa nia moja. Maana toka nchi iliyo mbali na mito ya Kushi, waniombao dua, yaani, binti za watu wangu waliotawanyika, wataleta matoleo yangu. Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu. Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la BWANA. Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya. Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli; Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu. BWANA ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye BWANA, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena. Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee. BWANA, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza katika upendo wake, Atakufurahia kwa kuimba. Nitawakusanya wanaousikitikia mkutano wa ibada, hao waliokuwa wa kwako; ambao mzigo uliokuwa juu yake ulikuwa fedheha kwao. Tazama, wakati huo nitawapatiliza watu wote wanaokutesa; nami nitamponya yeye achechemeaye, nami nitamkusanya yeye aliyefukuzwa; nami nitawafanya kuwa sifa na jina, hao ambao fedheha yao ilikuwa katika dunia yote. Wakati huo nitawaingizeni, na wakati huo nitawakusanya; kwa maana nitawafanya ninyi kuwa sifa na jina, miongoni mwa watu wote wa dunia, nitakapowarudisha wafungwa wenu mbele ya macho yenu, asema BWANA.

Shirikisha
Soma Sefania 3

Sefania 3:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Ole mji wa wadhalimu, waasi na waliotiwa unajisi! Hautii mtu yeyote, haukubali maonyo. Haumtumaini BWANA, haukaribii karibu na Mungu wake. Maafisa wake ni simba wanaonguruma, watawala wake ni mbwa-mwitu wa jioni, ambao hawabakizi chochote kwa ajili ya asubuhi. Manabii wake ni wenye kiburi, ni wadanganyifu. Makuhani wake hunajisi patakatifu na kuihalifu sheria. BWANA aliye ndani yake ni mwenye haki, hafanyi kosa. Asubuhi kwa asubuhi hutoa haki yake, kila kukipambazuka huitimiza, bali mtu dhalimu hana aibu. “Nimeyaangamiza mataifa, ngome zao zimebomolewa. Nimeziacha barabara ukiwa, hakuna anayepita humo. Miji yao imeharibiwa; hakuna mmoja atakayeachwa: hakuna hata mmoja. Niliuambia huo mji, ‘Hakika utaniogopa na kukubali maonyo!’ Ndipo makao yake hayatafutiliwa mbali, wala adhabu zangu zote hazitakuja juu yake. Lakini walikuwa bado na shauku kutenda kwa upotovu katika yote waliyofanya.” BWANA anasema, “Kwa hiyo ningojee mimi, siku nitakayosimama kuteka nyara. Nimeamua kukusanya mataifa, kukusanya falme na kumimina ghadhabu yangu juu yao, hasira yangu kali yote. Dunia yote itateketezwa kwa moto wa hasira yangu yenye wivu. “Ndipo nitatakasa midomo ya mataifa, kwamba wote waweze kuliitia jina la BWANA na kumtumikia kwa pamoja. Kutoka ngʼambo ya mito ya Kushi watu wangu wanaoniabudu, watu wangu waliotawanyika, wataniletea sadaka. Siku hiyo hutaaibishwa kwa ajili ya makosa yote uliyonitendea, kwa sababu nitawaondoa kutoka mji huu wale wote wanaoshangilia katika kiburi chao. Kamwe hutajivuna tena katika kilima changu kitakatifu. Lakini nitakuachia ndani yako wapole na wanyenyekevu, ambao wanatumaini jina la BWANA. Mabaki ya Israeli hayatafanya kosa; hawatasema uongo, wala udanganyifu hautakuwa katika vinywa vyao. Watakula na kulala wala hakuna yeyote atakayewaogopesha.” Imba, ee Binti Sayuni; paza sauti, ee Israeli! Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee Binti Yerusalemu! BWANA amekuondolea adhabu yako, amewarudisha nyuma adui zako. BWANA, Mfalme wa Israeli, yu pamoja nawe; kamwe hutaogopa tena madhara yoyote. Katika siku hiyo watauambia Yerusalemu, “Usiogope, ee Sayuni; usiiache mikono yako ilegee. BWANA Mungu wako yu pamoja nawe, yeye ni Shujaa mwenye nguvu anayeokoa. Atakufurahia kwa furaha kubwa, atakutuliza kwa pendo lake, atakufurahia kwa kuimba.” “Huzuni katika sikukuu zilizoamriwa nitaziondoa kwenu; hizo ni mzigo na fedheha kwenu. Wakati huo nitawaadhibu wote waliokudhulumu; nitaokoa vilema na kukusanya wale waliotawanywa. Nitawapa sifa na heshima katika kila nchi ambayo waliaibishwa. Wakati huo nitawakusanya; wakati huo nitawaleta nyumbani. Nitawapa sifa na heshima miongoni mwa mataifa yote ya dunia wakati nitakapowarudishia mateka yenu mbele ya macho yenu hasa,” asema BWANA.

Shirikisha
Soma Sefania 3