Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zekaria 9:1-17

Zekaria 9:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Kauli ya Mwenyezi-Mungu: Mwenyezi-Mungu ametamka siyo tu dhidi ya nchi ya Hadraki bali pia dhidi ya Damasko. Maana nchi ya Aramu ni mali ya Mwenyezi-Mungu, kama vile yalivyo makabila yote ya Israeli. Hali kadhalika mji wa Hamathi unaopakana na Hadraki; na hata miji ya Tiro na Sidoni ingawaje yajiona kuwa na hekima sana. Mji wa Tiro umejijengea ngome kumbwa, umejirundikia fedha kama vumbi, na dhahabu kama takataka barabarani. Lakini Bwana ataichukua mali yake yote, utajiri wake atautumbukiza baharini, na kuuteketeza mji huo kwa moto. Mji wa Ashkeloni utaona hayo na kuogopa, nao mji wa Gaza utagaagaa kwa uchungu; hata Ekroni, maana tumaini lake litatoweka. Mji wa Gaza utapoteza mfalme wake, nao Ashkeloni hautakaliwa na watu. Mji wa Ashdodi utakaliwa na machotara. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Kiburi cha Filistia nitakikomesha. Nitawakomesha kula nyama yenye damu, na chakula ambacho ni chukizo. Mabaki watakuwa mali yangu, kama ukoo mmoja katika Yuda. Watu wa Ekroni watakuwa kama Wayebusi. Mimi mwenyewe nitailinda nchi yangu, nitazuia majeshi yasipitepite humo. Hakuna mtu atakayewadhulumu tena watu wangu, maana, kwa macho yangu mwenyewe, nimeona jinsi walivyoteseka.” Shangilieni sana enyi watu wa Siyoni! Paazeni sauti, enyi watu wa Yerusalemu! Tazama, mfalme wenu anawajieni, anakuja kwa shangwe na ushindi! Ni mpole, amepanda punda, mwanapunda, mtoto wa punda. Atatokomeza magari ya vita nchini Efraimu, na farasi wa vita kutoka mjini Yerusalemu; pinde za vita zitavunjiliwa mbali. Naye ataleta amani miongoni mwa mataifa; utawala wake utaenea toka bahari hata bahari, toka mto Eufrate hata miisho ya dunia. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Kwa sababu ya agano langu nanyi, agano lililothibitishwa kwa damu, nitawakomboa wafungwa wenu walio kama wamefungwa katika shimo tupu. Enyi wafungwa wenye tumaini; rudini kwenye ngome yenu. Sasa mimi ninawatangazieni: Nitawarudishieni mema maradufu. Yuda nitamtumia kama uta wangu; Efraimu nimemfanya mshale wangu. Ee Siyoni! Watu wako nitawatumia kama upanga kuwashambulia watu wa Ugiriki; watakuwa kama upanga wa shujaa.” Mwenyezi-Mungu atawatokea watu wake; atafyatua mishale yake kama umeme. Bwana Mwenyezi-Mungu atapiga tarumbeta; atafika pamoja na kimbunga cha kusini. Mwenyezi-Mungu wa majeshi atawalinda watu wake, nao watawaangamiza maadui zao. Watapiga kelele vitani kama walevi wataimwaga damu ya maadui zao. Itatiririka kama damu ya tambiko iliyomiminwa madhabahuni kutoka bakulini. Wakati huo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, atawaokoa, maana wao ni kundi lake; nao watang'aa katika nchi yake kama mawe ya thamani katika taji. Jinsi gani uzuri na urembo wake ulivyo! Wavulana na wasichana watanawiri kwa wingi wa nafaka na divai mpya.

Shirikisha
Soma Zekaria 9

Zekaria 9:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ufunuo wa neno la BWANA, lililosemwa juu ya nchi ya Hadraki, na Dameski itakuwa mahali pake pa kustarehe; kwa maana jicho la mwanadamu na la kabila zote za Israeli linamwelekea BWANA; na Hamathi pia iliyo mpakani mwake; na Tiro, na Sidoni, kwa maana ana akili nyingi. Na Tiro alijijengea ngome, akakusanya fedha kama mchanga, dhahabu safi kama matope ya njia kuu. Tazama, Bwana atamwondolea mali zake, naye ataupiga uwezo wake alio nao baharini, naye mwenyewe atateketezwa kwa moto. Ashkeloni ataona haya na kuogopa; Gaza pia, naye atafadhaika sana; na Ekroni, kwa maana matarajio yake yatatahayarika; na mfalme ataangamia toka Gaza, na Ashkeloni atakuwa hana watu. Na mwana wa haramu atatawala huko Ashdodi, nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti. Nami nitaondoa damu yake kinywani mwake, na machukizo yake nitayatoa katika meno yake; yeye naye atakuwa ni mabaki kwa Mungu wetu; naye atakuwa kama mtu mkuu katika Yuda, na Ekroni kama Myebusi. Nami nitapiga kambi yangu pande zote za nyumba yangu ili kuwapinga adui, mtu awaye yote asipite ndani yake wala kurudi; wala mtu aoneaye hatapita tena kati yao; kwa maana sasa nimeona kwa macho yangu. Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwanapunda, mtoto wa punda. Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiria mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia. Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo na maji. Rudini katika ngome yenu, enyi wafungwa wa tumaini; hata hivi leo nasema ya kwamba nitakurudishia maradufu. Maana nimejipindia Yuda, nimeujaza upinde wangu Efraimu; nami nitawachochea wana wako, Ee Sayuni, wapigane na wana wako, Ee Ugiriki, nami nitakufanya wewe kuwa kama upanga wa shujaa. Naye BWANA ataonekana juu yao, Na mshale wake utatoka kama umeme; Na Bwana MUNGU ataipiga tarumbeta, Naye atakwenda kwa pepo za kisulisuli za kusini. BWANA wa majeshi atawalinda; Nao watakula na kuyakanyaga mawe ya teo; Nao watakunywa na kufanya kelele kama kwa divai; Nao watajazwa kama mabakuli, kama pembe za madhabahu. Na BWANA, Mungu wao, atawaokoa siku hiyo, Kama kundi la watu wake; Kwa maana watakuwa kama vito vya taji, Vikimetameta juu ya nchi yake. Maana wema wake, jinsi ulivyo mwingi! Na uzuri wake, jinsi ulivyo mwingi! Nafaka itawasitawisha vijana wanaume, Na divai mpya vijana wanawake.

Shirikisha
Soma Zekaria 9

Zekaria 9:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ufunuo wa neno la BWANA, lililosemwa juu ya nchi ya Hadraki, na Dameski itakuwa mahali pake pa kustarehe; kwa maana jicho la mwanadamu na la kabila zote za Israeli linamwelekea BWANA; na Hamathi pia iliyo mpakani mwake; na Tiro, na Sidoni, kwa maana ana akili nyingi. Na Tiro alijijengea ngome, akakusanya fedha kama mchanga, dhahabu safi kama matope ya njia kuu. Tazama, Bwana atamwondolea mali zake, naye ataupiga uwezo wake alio nao baharini, naye mwenyewe atateketezwa kwa moto. Ashkeloni ataona haya na kuogopa; Gaza pia, naye atafadhaika sana; na Ekroni, kwa maana taraja lake litatahayarika; na mfalme ataangamia toka Gaza, na Ashkeloni atakuwa hana watu. Na mwana wa haramu atatawala huko Ashdodi, nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti. Nami nitaondoa damu yake kinywani mwake, na machukizo yake nitayatoa katika meno yake; yeye naye atakuwa ni mabaki kwa Mungu wetu; naye atakuwa kama mtu mkuu katika Yuda, na Ekroni kama Myebusi. Nami nitapiga kambi yangu pande zote za nyumba yangu ili kuwapinga adui, mtu awaye yote asipite ndani yake wala kurudi; wala mtu aoneaye hatapita tena kati yao; kwa maana sasa nimeona kwa macho yangu. Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda. Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiri mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia. Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo na maji. Irudieni ngome, enyi wafungwa wa tumaini; hata hivi leo nasema ya kwamba nitakurudishia maradufu. Maana nimejipindia Yuda, nimeujaza upinde wangu Efraimu; nami nitawaondokesha wana wako, Ee Sayuni, wapigane na wana wako, Ee Uyunani, nami nitakufanya wewe kuwa kama upanga wa shujaa. Naye BWANA ataonekana juu yao, Na mshale wake utatoka kama umeme; Na Bwana MUNGU ataipiga tarumbeta, Naye atakwenda kwa pepo za kisulisuli za kusini. BWANA wa majeshi atawalinda; Nao watakula na kuyakanyaga mawe ya teo; Nao watakunywa na kufanya kelele kama kwa divai; Nao watajazwa kama mabakuli, kama pembe za madhabahu. Na BWANA, Mungu wao, atawaokoa siku hiyo, Kama kundi la watu wake; Kwa maana watakuwa kama vito vya taji, Vikimeta-meta juu ya nchi yake. Maana wema wake, jinsi ulivyo mwingi! Na uzuri wake, jinsi ulivyo mwingi! Nafaka itawasitawisha vijana wanaume, Na divai mpya vijana wanawake.

Shirikisha
Soma Zekaria 9

Zekaria 9:1-17 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Neno la unabii: Neno la BWANA liko kinyume na nchi ya Hadraki na Dameski itakuwa mahali pa kupumzika, kwa kuwa macho ya watu na ya makabila yote ya Israeli yako kwa BWANA; pia juu ya Hamathi inayopakana nayo, juu ya Tiro na Sidoni, ingawa wana ujuzi mwingi sana. Tiro amejijengea ngome imara, amelundika fedha kama mavumbi, na dhahabu kama taka za mitaani. Lakini Bwana atamwondolea mali yake na kuuangamiza uwezo wake wa baharini, naye atateketezwa kwa moto. Ashkeloni ataona hili na kuogopa; Gaza atagaagaa kwa maumivu makali, pia Ekroni, kwa sababu matumaini yake yatanyauka. Gaza atampoteza mfalme wake na Ashkeloni ataachwa pweke. Wageni watakalia mji wa Ashdodi, nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti. Nitaondoa damu vinywani mwao, chakula kile walichokatazwa kati ya meno yao. Mabaki yao yatakuwa mali ya Mungu wetu, nao watakuwa viongozi katika Yuda, naye Ekroni atakuwa kama Wayebusi. Lakini nitailinda nyumba yangu dhidi ya majeshi ya wanyangʼanyi. Kamwe mdhalimu hatashambulia watu wangu tena, kwa maana sasa ninawachunga. Shangilia sana, ee Binti Sayuni! Piga kelele, Binti Yerusalemu! Tazama, Mfalme wako anakuja kwako, ni mwenye haki, naye ana wokovu, ni mpole, naye amepanda punda, mwana-punda, mtoto wa punda. Nitaondoa magari ya vita kutoka Efraimu na farasi wa vita kutoka Yerusalemu, nao upinde wa vita utavunjwa. Atatangaza amani kwa mataifa. Utawala wake utaenea kutoka bahari hadi bahari, na kutoka Mto hadi mwisho wa dunia. Kwako wewe, kwa sababu ya damu ya agano langu nawe, nitawaacha huru wafungwa wako watoke kwenye shimo lisilo na maji. Rudieni ngome yenu, enyi wafungwa wa tumaini; hata sasa ninatangaza kwamba nitawarejesheeni maradufu. Nitampinda Yuda kama nipindavyo upinde wangu, nitamfanya Efraimu mshale wangu. Nitawainua wana wako, ee Sayuni, dhidi ya wana wako, ee Uyunani, na kukufanya kama upanga wa shujaa wa vita. BWANA Kisha BWANA atawatokea; mshale wake utamulika kama radi. BWANA Mwenyezi atapiga tarumbeta, naye atatembea katika tufani za kusini, na BWANA wa majeshi atawalinda. Wataangamiza na kushinda kwa mawe ya kutupa kwa kombeo. Watakunywa na kunguruma kama waliolewa mvinyo; watajaa kama bakuli linalotumika kunyunyizia kwenye pembe za madhabahu. BWANA Mungu wao atawaokoa siku hiyo kama kundi la watu wake. Watangʼara katika nchi yake kama vito vya thamani kwenye taji. Jinsi gani watavutia na kuwa wazuri! Nafaka itawastawisha vijana wanaume, nayo divai mpya vijana wanawake.

Shirikisha
Soma Zekaria 9