Zekaria 7:8-14
Zekaria 7:8-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mimi Zekaria: “Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema: Amueni kwa haki, muwe na upole na huruma nyinyi kwa nyinyi. Msiwadhulumu wajane, yatima, wageni au maskini; msikusudie mabaya mioyoni mwenu dhidi yenu wenyewe. “Lakini watu walikataa kunisikiliza, wakakaidi na kuziba masikio yao ili wasisikie. Wakaifanya mioyo yao kuwa migumu kama jiwe, wasije wakasikia sheria yangu mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi niliyoitangaza kwa roho yangu kwa kupitia manabii waliotangulia. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nikawaka hasira dhidi yao, nikasema, ‘Kwa kuwa niliwaita nao hawakunisikiliza, basi, nao waliponiita, sikuwasikiliza. Nami niliwatawanya kwa kimbunga kati ya mataifa yote ambayo hawakuyajua. Hivyo nchi waliyoiacha ikabaki tupu; hapakuwa na mtu yeyote aliyekaa humo; naam, nchi hiyo ya kupendeza ikawa ukiwa.’”
Zekaria 7:8-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha neno la BWANA likamjia Zekaria, kusema, BWANA wa majeshi amesema hivi, ya kwamba, Fanyeni hukumu za kweli, kila mtu na amwonee ndugu yake rehema na huruma; tena msimdhulumu mjane, wala yatima, wala mgeni, wala maskini; wala mtu awaye yote miongoni mwenu asiwaze mabaya juu ya ndugu yake moyoni mwake. Lakini hao walikataa kusikiliza, wakageuza bega lao, wakaziba masikio yao ili wasisikie. Naam, walifanya mioyo yao kuwa kama jiwe gumu, wasije wakaisikia sheria na maneno ya BWANA wa majeshi, aliyoyatuma kwa roho yake, kwa mkono wa manabii wa kwanza; kwa sababu hiyo ghadhabu kuu ikatoka kwa BWANA wa majeshi. Ikawa kama wakati nilipowaita, wasitake kunisikiliza; basi, nao wataniita, wala sitasikiliza, asema BWANA wa majeshi. Lakini nitawatawanya kwa kimbunga kikali katikati ya mataifa yote wasiyoyajua. Basi nchi walioacha ikawa ya ukiwa, hata hapakuwa na mtu aliyeipitia akienda wala akirudi; maana waliifanya nchi iliyopendeza kuwa ukiwa.
Zekaria 7:8-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha neno la BWANA likamjia Zekaria, kusema, BWANA wa majeshi amesema hivi, ya kwamba, Fanyeni hukumu za kweli, kila mtu na amwonee ndugu yake rehema na huruma; tena msimdhulumu mjane, wala yatima, wala mgeni, wala maskini; wala mtu awaye yote miongoni mwenu asiwaze mabaya juu ya ndugu yake moyoni mwake. Lakini hao walikataa kusikiliza, wakageuza bega lao, wakaziba masikio yao ili wasisikie. Naam, walifanya mioyo yao kuwa kama jiwe gumu, wasije wakaisikia sheria na maneno ya BWANA wa majeshi, aliyoyapeleka kwa roho yake kwa mkono wa manabii wa kwanza; kwa sababu hiyo ghadhabu kuu ikatoka kwa BWANA wa majeshi. Ikawa kwa sababu alilia, wao wasitake kusikiliza; basi, wao nao watalia, wala mimi sitasikiliza, asema BWANA wa majeshi. Lakini nitawatawanya kwa upepo wa kisulisuli, katikati ya mataifa yote wasiowajua. Basi hivyo ndivyo ilivyokuwa ukiwa nchi baada yao, hata hapakuwa na mtu aliyepita kati yake, wala aliyerudi; maana waliifanya nchi iliyopendeza sana kuwa ukiwa.
Zekaria 7:8-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Neno la BWANA likamjia tena Zekaria: “Hivi ndivyo asemavyo BWANA wa majeshi: ‘Fanyeni hukumu za haki, onesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi. Msimdhulumu mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’ “Lakini wakakataa kusikiliza, wakanipa kisogo kwa ukaidi na kuziba masikio yao. Wakaifanya mioyo yao migumu kama gumegume, na hawakuisikiliza sheria au maneno ambayo BWANA wa majeshi aliyatuma kwa Roho wake kupitia manabii waliotangulia. Kwa hiyo BWANA wa majeshi alikasirika sana. “ ‘Nilipoita, hawakusikiliza; kwa hiyo walipoita, sikusikiliza,’ asema BWANA wa majeshi. ‘Niliwatawanya kwa upepo wa kisulisuli miongoni mwa mataifa yote, mahali ambapo walikuwa wageni. Nchi ikaachwa ukiwa nyuma yao kiasi kwamba hakuna aliyeweza kuingia au kutoka. Hivi ndivyo walivyoifanya ile nchi iliyokuwa imependeza kuwa ukiwa.’ ”