Zekaria 6:1-15
Zekaria 6:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Niliona maono mengine tena. Safari hii, niliona magari manne ya farasi yakitoka katikati ya milima miwili ya shaba nyeusi. Gari la kwanza lilikokotwa na farasi wekundu, la pili lilikokotwa na farasi weusi, la tatu lilikokotwa na farasi weupe, na la nne lilikokotwa na farasi wa kijivujivu. Basi, nikamwuliza yule malaika aliyeongea nami, “Bwana, magari haya ya farasi yanamaanisha nini?” Malaika akanijibu, “Magari haya ni pepo kutoka pande nne za mbingu. Yalikuwa mbele ya Mwenyezi-Mungu wa dunia nzima, na sasa yanaondoka. Lile gari linalokokotwa na farasi weusi linakwenda kaskazini, lile linalokokotwa na farasi weupe linakwenda magharibi, na lile linalokokotwa na farasi wa kijivujivu linakwenda kusini.” Farasi hao walipotokea walikuwa na hamu sana ya kwenda kuikagua dunia. Naye malaika akawaambia, “Haya! Nendeni mkaikague dunia.” Basi, wakaenda na kuikagua dunia. Kisha yule malaika aliyeongea nami akaniambia kwa sauti, “Tazama! Wale farasi waliokwenda nchi ya kaskazini wameituliza ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.” Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Pokea zawadi za watu walio uhamishoni zilizoletwa na Heldai, Tobia na Yedaya. Nenda leo hii nyumbani kwa Yosia, mwana wa Sefania ambamo watu hao wamekwenda baada ya kuwasili kutoka Babuloni. Utachukua fedha na dhahabu hiyo, utengeneze taji ambalo utamvika kuhani mkuu Yoshua, mwana wa Yehosadaki, na kumwambia kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Hapa pana mtu aitwaye Tawi. Yeye atastawi hapo alipo na kulijenga hekalu langu mimi Mwenyezi-Mungu. Yeye ndiye atakayelijenga hekalu langu mimi Mwenyezi-Mungu Atapewa heshima ya kifalme na kuketi kwenye kiti chake cha enzi kuwatawala watu wake. Karibu na kiti cha enzi cha mtawala huyo, atakaa kuhani mkuu, nao wawili watafanya kazi pamoja kwa amani. Taji hilo itahifadhiwa katika hekalu langu kwa heshima ya Heldai, Tobia, Yedaya na Yosia mwana wa Sefania.’ “Watu wanaokaa nchi za mbali watakuja kusaidia kulijenga hekalu langu mimi Mwenyezi-Mungu.” Nanyi mtajua kwamba Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ndiye aliyenituma kwenu. Haya yote yatatukia kama mkiitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
Zekaria 6:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, yanatokea magari ya vita manne, yanatoka kati ya milima miwili, na milima hiyo ilikuwa ni milima ya shaba. Katika gari la kwanza walikuwa farasi wekundu; na katika gari la pili walikuwa farasi weusi; na katika gari la tatu walikuwa farasi weupe; na katika gari la nne walikuwa farasi wa rangi ya kijivujivu. Nikajibu, nikamwuliza yule malaika aliyesema nami, Hawa ni nini, Bwana wangu? Malaika akajibu, akaniambia, Hawa ni pepo nne za mbinguni, zitokeazo baada ya kusimama mbele za Bwana wa dunia yote. Gari lile lenye farasi weusi latoka kwenda hata nchi ya kaskazini; nao farasi weupe wanatoka kwenda katika nchi ya magharibi; na wale wa rangi ya kijivujivu wakatoka kwenda hadi nchi ya kusini. Farasi wale walipotoka, walitaka kwenda huku na huko katika dunia; naye akawaambia, Haya! Tokeni, mwende huku na huko katika dunia. Basi wakaenda huku na huko katika dunia. Ndipo akaniita, akaniambia akisema, Tazama, wale waendao mpaka nchi ya kaskazini wameituliza roho yangu katika nchi ya kaskazini. Neno la BWANA likanijia, kusema, Pokea vitu mikononi mwa baadhi ya watu waliohamishwa, yaani, Heldai, na Tobia, na Yedaya; na siku iyo hiyo nenda ukaingie katika nyumba ya Yosia, mwana wa Sefania, waliyoifikia kutoka Babeli; naam, pokea fedha na dhahabu, ukatengeneze taji, ukamvike kichwani Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu; ukamwambie, ukisema, BWANA wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Tazama, mtu huyu ndiye ambaye jina lake ni Chipukizi; naye atakua katika mahali pake, naye atalijenga hekalu la BWANA. Naam, yeye atalijenga hekalu la BWANA; naye atakuwa na heshima ya kifalme; na ataketi na kutawala; na kutakuwa na kuhani katika kiti chake cha enzi; na maelewano yenye amani yatakuwa kati ya hao wawili. Na hayo mataji yatakuwa ya Heldai, na Tobia, na Yedaya; na kwa fadhili za mwana wa Sefania; yawe kumbukumbu katika hekalu la BWANA. Nao walio mbali watakuja na kusaidia kujenga hekalu la BWANA, nanyi mtajua ya kuwa BWANA wa majeshi amenituma kwenu. Na haya yatatokea, kama mkijitahidi kuitii sauti ya BWANA, Mungu wenu.
Zekaria 6:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, yanatokea magari ya vita manne, yanatoka kati ya milima miwili, na milima hiyo ilikuwa ni milima ya shaba. Katika gari la kwanza walikuwa farasi wekundu; na katika gari la pili walikuwa farasi weusi; na katika gari la tatu walikuwa farasi weupe; na katika gari la nne walikuwa farasi wa rangi ya kijivujivu. Nikajibu, nikamwuliza yule malaika aliyesema nami, Hawa ni nini, Bwana wangu? Malaika akajibu, akaniambia, Hawa ni pepo nne za mbinguni, zitokeazo baada ya kusimama mbele za Bwana wa dunia yote. Gari lile lenye farasi weusi latoka kwenda hata nchi ya kaskazini; nao farasi weupe wakatoka wakafuata nyuma yao; na wale wa rangi ya kijivujivu wakatoka kwenda hata nchi ya kusini. Na wale wekundu wakatoka, wakataka kwenda huko na huko katika dunia; naye akawaambia, Haya! Tokeni, mwende huko na huko katika dunia. Basi wakaenda huko na huko katika dunia. Ndipo akaniita, akaniambia akisema, Tazama, wale waendao mpaka nchi ya kaskazini wameituliza roho yangu katika nchi ya kaskazini. Neno la BWANA likanijia, kusema, Pokea vitu mikononi mwa baadhi ya watu waliohamishwa, yaani, Heldai, na Tobia, na Yedaya; na siku iyo hiyo enenda ukaingie katika nyumba ya Yosia, mwana wa Sefania, waliyoifikia kutoka Babeli; naam, pokea fedha na dhahabu, ukafanye taji, ukamvike kichwani Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu; ukamwambie, ukisema, BWANA wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Tazama, mtu huyu ndiye ambaye jina lake ni Chipukizi; naye atakua katika mahali pake, naye atalijenga hekalu la BWANA. Naam, yeye atalijenga hekalu la BWANA; naye atauchukua huo utukufu; ataketi akimiliki katika kiti chake cha enzi; na kutakuwa na kuhani katika kiti chake cha enzi; na shauri la amani litakuwa kati ya hao wawili. Na hizo taji zitakuwa za Heldai, na Tobia, na Yedaya; na kwa fadhili za mwana wa Sefania; ziwe ukumbusho katika hekalu la BWANA. Nao walio mbali watakuja na kujenga katika hekalu la BWANA, nanyi mtajua ya kuwa BWANA wa majeshi amenituma kwenu. Na haya yatatokea, kama mkijitahidi kuitii sauti ya BWANA, Mungu wenu.
Zekaria 6:1-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nikatazama juu tena: nikaona mbele yangu magari manne ya vita yakija kutoka kati ya milima miwili, milima ya shaba! Gari la kwanza lilivutwa na farasi wekundu, la pili lilivutwa na farasi weusi, la tatu lilivutwa na farasi weupe, na gari la nne lilivutwa na farasi wa madoadoa ya kijivu, wote wenye nguvu. Nikamuuliza malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Hawa ni nani, bwana wangu?” Malaika akanijibu, “Hizi ni roho nne za mbinguni zisimamazo mbele ya uwepo wa Bwana wa dunia yote, zinatoka kwenda kufanya kazi yake. Gari linalovutwa na farasi weusi linaelekea katika nchi ya kaskazini, la farasi weupe linaelekea magharibi, na la farasi wa madoadoa ya kijivu linaelekea kusini.” Hao farasi wenye nguvu walipokuwa wakitoka, walikuwa wakijitahidi kwenda duniani kote. Akasema, “Nenda duniani kote!” Kwa hiyo wakaenda duniani kote. Kisha akaniita, “Tazama, wale wanaoenda kuelekea nchi ya kaskazini wamepumzisha Roho wangu katika nchi ya kaskazini.” Neno la BWANA likanijia kusema: “Chukua fedha na dhahabu kutoka kwa watu waliohamishwa, yaani Heldai, Tobia na Yedaya ambao wamefika kutoka Babeli. Siku hiyo hiyo nenda nyumbani mwa Yosia mwana wa Sefania. Chukua fedha na dhahabu utengeneze taji, nawe uliweke kichwani mwa kuhani mkuu Yoshua, mwana wa Yehosadaki. Umwambie hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi: ‘Huyu ndiye mtu anayeitwa Tawi, naye atachipua kutoka mahali pake na kujenga Hekalu la BWANA. Ni yeye atakayejenga Hekalu la BWANA, naye atavikwa utukufu na ataketi kumiliki kwenye kiti cha enzi. Atakuwa kuhani kwenye kiti chake cha enzi. Hapo patakuwa na amani kati ya hao wawili.’ Taji litatolewa kwa Heldai, Tobia, Yedaya na Heni mwana wa Sefania kama kumbukumbu ndani ya Hekalu la BWANA. Wale walio mbali sana watakuja na kusaidia kulijenga Hekalu la BWANA, nanyi mtajua kuwa BWANA wa majeshi amenituma kwenu. Hili litatokea ikiwa mtamtii BWANA Mungu wenu kwa bidii.”