Zekaria 5:1-11
Zekaria 5:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Nilipotazama tena niliona kitabu kinaruka angani. Yule malaika akaniuliza, “Unaona nini?” Nami nikamjibu, “Ninaona kitabu kinaruka angani; urefu wake ni mita tisa na upana wake ni mita nne na nusu.” Basi, yeye akaniambia, “Ndani ya kitabu hicho kumeandikwa laana ambayo itaikumba nchi nzima. Upande mmoja imeandikwa kwamba wezi wote watafukuzwa nchini, na upande mwingine imeandikwa kwamba wote wenye kuapa uongo kadhalika watafanyiwa vivyo hivyo. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema kuwa yeye mwenyewe ataipeleka laana hiyo. Itapenya kila nyumba ya mwizi na kila nyumba ya mwenye kuapa uongo kwa kutumia jina lake; itakaa humo na kuteketeza nyumba hiyo yote, mbao na mawe.” Yule malaika aliyeongea nami alinikaribia, akaniambia, “Hebu tazama uone kile kinachokuja.” Nami nikamwuliza, “Ni kitu gani hicho?” Naye akanijibu, “Hicho ni kikapu chenye makosa ya nchi nzima.” Kikapu chenyewe kilikuwa na mfuniko uliotengenezwa kwa risasi; kilifunuliwa, nami nikaona mwanamke ameketi humo ndani. Yule malaika akaniambia, “Mwanamke huyo anawakilisha uovu!” Kisha huyo malaika akamsukumia ndani ya kikapu mwanamke huyo na kukifunika. Nilipotazama juu, niliona wanawake wawili wanatokea kunijia; walikuwa wakirushwa na upepo, nao walikuwa na mabawa yenye nguvu kama ya korongo. Wanawake hao wakakiinua kile kikapu angani. Basi, nikamwuliza yule malaika aliyezungumza nami, “Wanakipeleka wapi kile kikapu?” Naye akaniambia “Wanakipeleka katika nchi ya Shinari. Huko watakijengea hekalu na litakapokuwa tayari, watakiweka kikapu hicho ndani.”
Zekaria 5:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, gombo la kitabu lirukalo. Akaniuliza, Unaona nini? Nikajibu, Naona gombo la kitabu lirukalo; na urefu wake ni dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa kumi. Ndipo akaniambia, Hii ndiyo laana itokayo kwenda juu ya uso wa nchi yote; maana kwa hiyo kila aibaye atakatiwa mbali kama ilivyoandikwa upande, na kwa hiyo kila aapaye kwa uongo atakatiliwa mbali kama ilivyo andikwa upande wa pili. Nitaituma itokee, asema BWANA wa majeshi, nayo itaingia katika nyumba ya mwizi, na katika nyumba ya yeyote aapaye kwa uongo kwa jina langu; nayo itakaa katika nyumba yake, na kuiteketeza, pamoja na boriti zake na mawe yake. Ndipo yule malaika aliyesema nami akatokea, akaniambia, Inua macho yako sasa, uone ni kitu gani kitokeacho. Nikasema, Ni kitu gani? Akasema, Kitu hiki ni efa itokeayo. Tena akasema, Huu ndio uovu wao katika nchi hii yote; na tazama, kifuniko cha risasi kiliinuliwa; na tazama, mlikuwa na mwanamke ndani ya kikapu. Akasema, Huyu ni Uovu; akamsukuma ndani ya kile kikapu; akalitupa lile jiwe la risasi juu ya mdomo wa ile efa. Ndipo nikainua macho yangu, nikaona, na tazama, wanawake wawili walitokea, nao upepo ulikuwa katika mabawa yao; na mabawa yao yalikuwa kama mabawa ya korongo; wakaiinua ile efa kati ya dunia na mbingu. Ndipo nikamwambia yule malaika aliyesema nami, Hawa wanaipeleka wapi efa hii? Akaniambia, Wanakwenda kumjengea nyumba katika nchi ya Shinari; tena ikiisha kutengenezwa, atawekwa huko mahali pake mwenyewe.
Zekaria 5:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, gombo la chuo lirukalo. Akaniuliza, Unaona nini? Nikajibu, Naona gombo la chuo lirukalo; na urefu wake ni dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa kumi. Ndipo akaniambia, Hii ndiyo laana itokayo kwenda juu ya uso wa nchi yote; maana kwa hiyo kila aibaye atatolewa kama ilivyo upande mmoja, na kwa hiyo kila aapaye atatolewa kama ilivyo upande wa pili. Nitaituma itokee, asema BWANA wa majeshi, nayo itaingia katika nyumba ya mwivi, na katika nyumba yake yeye aapaye kwa uongo kwa jina langu; nayo itakaa katikati ya nyumba yake, na kuiteketeza, pamoja na boriti zake na mawe yake. Ndipo yule malaika aliyesema nami akatokea, akaniambia, Inua macho yako sasa, uone ni kitu gani kitokeacho. Nikasema, Ni kitu gani? Akasema, Kitu hiki ni efa itokeayo. Tena akasema, Huu ndio uovu wao katika nchi hii yote; na tazama, talanta ya risasi iliinuliwa; na tazama, mwanamke akaaye katikati ya hiyo efa. Akasema, Huyu ni Uovu; akamtupa chini katikati ya ile efa; akalitupa lile jiwe la risasi juu ya mdomo wa ile efa. Ndipo nikainua macho yangu, nikaona, na tazama, wanawake wawili walitokea, nao upepo ulikuwa katika mabawa yao; na mabawa yao yalikuwa kama mabawa ya korongo; wakaiinua ile efa kati ya dunia na mbingu. Ndipo nikamwambia yule malaika aliyesema nami, Hawa wanaipeleka wapi efa hii? Akaniambia, Wanakwenda kumjengea nyumba katika nchi ya Shinari; tena ikiisha kutengenezwa, atawekwa huko mahali pake mwenyewe.
Zekaria 5:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nikatazama tena: na hapo mbele yangu kulikuwa na kitabu kinachoruka! Akaniuliza, “Unaona nini?” Nikamjibu, “Naona kitabu kinachoruka, chenye urefu wa dhiraa ishirini, na upana wa dhiraa kumi.” Akaniambia, “Hii ni laana inayotoka kwenda juu ya nchi yote, kwa kuwa kufuatana na yale yaliyoandikwa katika upande mmoja, kila mwizi atafukuziwa mbali, pia kufuatana na yaliyo upande wa pili, kila aapaye kwa uongo atafukuziwa mbali. BWANA wa majeshi asema, ‘Nitaituma hiyo laana, nayo itaingia katika nyumba ya mwizi na nyumba ya huyo aapaye kwa uongo kwa Jina langu. Itabaki katika nyumba yake na kuiharibu, pamoja na mbao zake na mawe yake.’ ” Kisha yule malaika aliyekuwa akizungumza nami akanijia na kuniambia, “Tazama juu uone ni nini kile kinachojitokeza.” Nikamuuliza, “Ni kitu gani?” Akanijibu, “Ni kikapu cha kupimia.” Kisha akaongeza kusema, “Huu ni uovu wa watu katika nchi nzima.” Kisha kifuniko kilichotengenezwa kwa madini ya risasi kilichokuwa kimefunika kile kikapu, kiliinuliwa na ndani ya kile kikapu alikuwako mwanamke ameketi! Akasema, “Huu ni uovu,” tena akamsukumia ndani ya kikapu na kushindilia kifuniko juu ya mdomo wa kikapu. Kisha nikatazama juu: na pale mbele yangu, palikuwa na wanawake wawili, wakiwa na upepo katika mabawa yao! Walikuwa na mabawa kama ya korongo, nao wakainua kile kikapu na kuruka nacho kati ya mbingu na nchi. Nikamuuliza yule malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Wanakipeleka wapi hicho kikapu?” Akanijibu, “Wanakipeleka katika nchi ya Babeli na kujenga nyumba kwa ajili yake. Itakapokuwa tayari, kikapu kitawekwa pale mahali pake.”