Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zekaria 3:1-10

Zekaria 3:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

Katika maono mengine, Mwenyezi-Mungu alinionesha kuhani mkuu Yoshua amesimama mbele ya malaika wa Mwenyezi-Mungu, na upande wake wa kulia amesimama Shetani kumshtaki. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia huyo Shetani, “Mwenyezi-Mungu na akulaani, ewe Shetani! Naam, Mwenyezi-Mungu aliyeuteua mji wa Yerusalemu na akulaani! Mtu huyu ni kama kinga kilichonyakuliwa kutoka motoni!” Kuhani mkuu Yoshua alikuwa amesimama mbele ya malaika, akiwa amevaa mavazi machafu. Malaika akawaambia watumishi wake, “Mvueni kuhani mkuu Yoshua mavazi yake machafu.” Kisha akamwambia kuhani mkuu Yoshua, “Tazama, nimeiondoa dhambi yako, nami nitakupa mavazi ya thamani.” Kisha akawaambia wamvike kilemba safi kichwani. Hivyo, wakamvika kilemba safi na mavazi; naye malaika wa Mwenyezi-Mungu alikuwa amesimama hapo. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwonya kuhani mkuu Yoshua, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Ukifuata mwongozo wangu na kuyazingatia maagizo niliyokupa, basi, utaisimamia nyumba yangu na nyua zake. Nami nitakuwezesha kuingia katika utumishi wangu kama hawa wanaosimama mbele yangu. Sasa sikiliza kwa makini, ewe Yoshua, kuhani mkuu; sikilizeni pia enyi makuhani wenzake mlio pamoja naye, nyinyi mlio ishara ya wakati mzuri ujao: Nitamleta mtumishi wangu aitwaye Tawi. Kumbukeni kuwa nimeweka mbele ya Yoshua jiwe moja lenye nyuso saba. Nami nitachora maandishi juu yake, na kwa siku moja tu, nitaiondoa dhambi ya nchi hii. Naam, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. Siku hiyo, kila mmoja wenu atamwalika mwenzake kufurahia amani na utulivu katika shamba lake la mizabibu na la mitini.’”

Shirikisha
Soma Zekaria 3

Zekaria 3:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha akanionesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa BWANA, na Shetani amesimama mkono wake wa kulia ili kushindana naye. BWANA akamwambia Shetani, BWANA na akukemee Ewe Shetani; naam, BWANA, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je, Hiki si kinga kilichotolewa motoni? Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya malaika. Naye malaika akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi chafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani kubwa. Nikasema, Na wampige kilemba kizuri kichwani pake. Basi, wakampiga kilemba kizuri kichwani pake, wakamvika mavazi; naye malaika wa BWANA akasimama karibu. Kisha malaika wa BWANA akamshuhudia Yoshua, akisema, BWANA wa majeshi asema hivi, Ikiwa utaenda katika njia zangu, na kushika maagizo yangu, basi utaihukumu nyumba yangu, na kuzilinda nyua zangu, nami nitakupa haki ya kunikaribia kati yao wasimamao karibu. Sikiliza sasa, Ee Yoshua, kuhani mkuu, wewe na wenzako wanaoketi mbele yako; maana hao ni watu walio ishara ya mambo yajayo; kwa maana, tazama, ninamleta mtumishi wangu, aitwaye Chipukizi. Maana, litazame jiwe hili nililoliweka mbele ya Yoshua; katika jiwe moja ziko nyuso saba; tazama, nitachonga maandishi yake, asema BWANA wa majeshi, nami nitauondoa uovu wa nchi hii katika siku moja. Katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, ninyi mtamwalika kila mtu jirani yake chini ya mzabibu, na chini ya mtini.

Shirikisha
Soma Zekaria 3

Zekaria 3:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa BWANA, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye. BWANA akamwambia Shetani, BWANA na akukemee Ewe Shetani; naam, BWANA, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni? Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya malaika. Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi. Nikasema, Na wampige kilemba kizuri kichwani pake. Basi, wakampiga kilemba kizuri kichwani pake, wakamvika mavazi; naye malaika wa BWANA akasimama karibu. Kisha malaika wa BWANA akamshuhudia Yoshua, akisema, BWANA wa majeshi asema hivi, Kama ukienda katika njia zangu, na kama ukishika maagizo yangu, ndipo utakapoihukumu nyumba yangu, nawe utazilinda nyua zangu, nami nitakupa nafasi ya kunikaribia kati yao wasimamao karibu. Sikiliza sasa, Ee Yoshua, kuhani mkuu, wewe na wenzako waketio mbele yako; maana hao ni watu walio ishara; kwa maana, tazama, ninamleta mtumishi wangu, aitwaye Chipukizi. Maana, litazame jiwe hili nililoliweka mbele ya Yoshua; katika jiwe moja yako macho saba; tazama, nitachora machoro yake, asema BWANA wa majeshi, nami nitauondoa uovu wa nchi ile katika siku moja. Katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, ninyi mtamwalika kila mtu jirani yake chini ya mzabibu, na chini ya mtini.

Shirikisha
Soma Zekaria 3

Zekaria 3:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Kisha akanionesha Yoshua, kuhani mkuu, akiwa amesimama mbele ya malaika wa BWANA, naye Shetani amesimama upande wake wa kuume ili amshtaki. BWANA akamwambia Shetani, “BWANA akukemee Shetani! BWANA, ambaye ameichagua Yerusalemu, akukemee! Je, mtu huyu siyo kijinga kinachowaka kilichonyakuliwa kwenye moto?” Wakati huu, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu alipokuwa amesimama mbele ya malaika. Malaika akawaambia wale waliokuwa wamesimama mbele yake, “Mvueni hizo nguo zake chafu.” Kisha akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeiondoa dhambi yako, nami nitakuvika mavazi ya kitajiri.” Kisha nikasema, “Mvike kilemba kilicho safi kichwani mwake.” Kwa hiyo wakamvika kilemba safi kichwani na kumvika yale mavazi mengine, wakati malaika wa BWANA akiwa amesimama karibu. Malaika wa BWANA akamwamuru Yoshua: “Hivi ndivyo asemavyo BWANA wa majeshi: ‘Ikiwa utatembea katika njia zangu na kushika maagizo yangu, basi utaitawala nyumba yangu na kuzilinda nyua zangu, nami nitakupa nafasi miongoni mwa hawa wasimamao hapa. “ ‘Sikiliza, ee Yoshua kuhani mkuu, pamoja na wenzako walioketi mbele yako, ambao ni watu walio ishara ya mambo yatakayokuja: Ninaenda kumleta mtumishi wangu, Tawi. Tazama, jiwe nililoliweka mbele ya Yoshua! Kuna macho saba juu ya jiwe lile moja, nami nitachora maandishi juu yake,’ asema BWANA wa majeshi, ‘nami nitaiondoa dhambi ya nchi hii kwa siku moja. “ ‘Katika siku hiyo kila mmoja wenu atamwalika jirani yake akae chini ya mzabibu wake na mtini wake,’ asema BWANA wa majeshi.”

Shirikisha
Soma Zekaria 3