Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zekaria 10:1-12

Zekaria 10:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwombeni Mwenyezi-Mungu awape mvua za masika. Mwenyezi-Mungu ndiye aletaye mawingu ya mvua; ndiye awapaye watu mvua za rasharasha, na kustawisha mimea shambani kwa ajili ya wote. Vinyago vyao vya kupigia ramli ni upuuzi mtupu, na waaguzi wao wanaagua uongo; watabiri wao wanatabiri ndoto za danganyifu, na kuwapa watu faraja tupu. Ndio maana watu wa Yuda wanatangatanga kama kondoo; wanataabika kwa kuwa wamekosa mchungaji. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nimewaka hasira dhidi ya hao wachungaji, nami nitawaadhibu hao viongozi. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nitalitunza kundi langu, ukoo wa Yuda. Nitawafanya kuwa farasi wangu hodari wa vita. Kwa ukoo wa Yuda kutatokea: Watawala wa kila namna, viongozi imara kama jiwe kuu la msingi, walio thabiti kama kigingi cha hema, wenye nguvu kama upinde wa vita. Watu wa Yuda watakuwa kama mashujaa vitani watawakanyaga maadui zao katika tope njiani. Watapigana kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nipo pamoja nao; nao watawaaibisha hata wapandafarasi. “Watu wa Yuda nitawaimarisha; nitawaokoa wazawa wa Yosefu. Nitawarejesha makwao kwa maana nawaonea huruma, nao watakuwa kana kwamba sikuwa nimewakataa. Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, nami nitayasikiliza maombi yao. Watu wa Efraimu watakuwa kama mashujaa vitani; watajaa furaha kama waliokunywa divai. Watoto wao wataona hayo na kufurahi, watajaa furaha mioyoni kwa sababu yangu Mwenyezi-Mungu. “Nitawaita watu wangu na kuwakusanya pamoja; nimekusudia kuwakomboa, nao watakuwa wengi kama hapo awali. Japo niliwatawanya kati ya mataifa, hata hivyo, watanikumbuka wakiwa humo. Nao pamoja na watoto wao wataishi na kurudi majumbani mwao. Nitawarudisha kutoka nchini Misri, nitawakusanya kutoka Ashuru; nitawaleta nchini Gileadi na Lebanoni, nao watajaa kila mahali nchini. Watapitia katika bahari ya mateso, nami nitayapiga mawimbi yake, na vilindi vya maji ya mto Nili vitakauka. Kiburi cha Ashuru kitavunjwa na nguvu za Misri zitatoweka. Mimi nitawaimarisha watu wangu, nao watanitii na kuishi kwa kunipendeza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Shirikisha
Soma Zekaria 10

Zekaria 10:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mwombeni BWANA mvua wakati wa masika, naam, BWANA aletaye mawingu ya mvua, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi shambani. Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo watu wanatangatanga kama kondoo, wanateseka kwa kukosa mchungaji. Hasira yangu imewaka juu ya wachungaji, nami nitawaadhibu viongozi; kwa maana BWANA wa majeshi ameliangalia kundi lake, yaani, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kuwa kama farasi wake mzuri vitani. Kwake yeye litatoka lile jiwe la pembeni, kwake yeye utatoka msumari, kwake yeye utatoka upinde wa vita, kwake yeye atatoka kila kamanda. Nao watakuwa kama mashujaa, wakanyagao adui zao katika matope ya njia vitani; nao watapiga vita, kwa sababu BWANA yu pamoja nao; na hao wapandao farasi watafadhaishwa. Nami nitaitia nguvu nyumba ya Yuda, nami nitaiokoa nyumba ya Yusufu, nami nitawarudisha, kwa maana nawaonea rehema; nao watakuwa kana kwamba sikuwatupa; kwa maana mimi ni BWANA, Mungu wao, nami nitawasikia. Na watu wa Efraimu watakuwa kama shujaa, na moyo wao utafurahi kana kwamba ni kwa divai; naam, watoto wao wataona mambo haya, na kufurahi; mioyo yao itamfurahia BWANA. Nitawapigia kelele, na kuwakusanya pamoja; kwa maana nimewakomboa; nao wataongezeka kama walivyokua hapo awali. Nami nitawapanda kama mbegu kati ya mataifa; nao watanikumbuka katika nchi zilizo mbali; nao watakaa pamoja na watoto wao; tena watarudi. Tena nitawarudisha toka nchi ya Misri, nitawakusanya na kuwatoa katika Ashuru; nami nitawaingiza katika nchi ya Gileadi na Lebanoni; hata pasiwe na nafasi ya kuwatosha. Naye atapita kati ya bahari ya mateso, na kuyapiga mawimbi ya bahari, na vilindi vyote vya mto Nile vitakauka; na kiburi cha Ashuru kitashushwa; na fimbo ya enzi ya Misri itatoweka. Nami nitawatia nguvu katika BWANA; nao watatembea huku na huko katika jina lake, asema BWANA.

Shirikisha
Soma Zekaria 10

Zekaria 10:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mwombeni BWANA mvua wakati wa masika, naam, BWANA afanyaye umeme, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi kondeni. Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo waenda zao kama kondoo, wateswa, kwa sababu hapana mchungaji. Hasira yangu imewaka juu ya wachungaji, nami nitawaadhibu mbuzi waume; kwa maana BWANA wa majeshi ameliangalia kundi lake, yaani, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kuwa kama farasi wake mzuri vitani. Kwake yeye litatoka lile jiwe la pembeni, kwake yeye utatoka msumari, kwake yeye utatoka upinde wa vita, kwake yeye atatoka kila mtawala pamoja. Nao watakuwa kama mashujaa, wakanyagao adui zao katika matope ya njia vitani; nao watapiga vita, kwa sababu BWANA yu pamoja nao; na hao wapandao farasi watafadhaishwa. Nami nitaitia nguvu nyumba ya Yuda, nami nitaiokoa nyumba ya Yusufu, nami nitawarudisha, kwa maana nawaonea rehema; nao watakuwa kana kwamba sikuwatupa; kwa maana mimi ni BWANA, Mungu wao, nami nitawasikia. Na watu wa Efraimu watakuwa kama shujaa, na moyo wao utafurahi kana kwamba ni kwa divai; naam, watoto wao wataona mambo haya, na kufurahi; mioyo yao itamfurahia BWANA. Nitawapigia kelele, na kuwakusanya pamoja; kwa maana nimewakomboa; nao wataongezeka kama walivyoongezeka. Nami nitawapanda kama mbegu kati ya mataifa; nao watanikumbuka katika nchi zilizo mbali; nao watakaa pamoja na watoto wao; tena watarudi. Tena nitawarudisha toka nchi ya Misri, nitawakusanya na kuwatoa katika Ashuru; nami nitawaingiza katika nchi ya Gileadi na Lebanoni; ila nafasi ya kuwatosha haitaonekana. Naye atapita kati ya bahari ya mateso, na kuyapiga mawimbi ya bahari, na vilindi vyote vya mto wa Nile vitakauka; na kiburi cha Ashuru kitashushwa; na fimbo ya enzi ya Misri itatoweka. Nami nitawatia nguvu katika BWANA; nao watatembea huko na huko katika jina lake, asema BWANA.

Shirikisha
Soma Zekaria 10

Zekaria 10:1-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Mwombeni BWANA mvua wakati wa vuli; ndiye BWANA atengenezaye mawingu ya tufani. Huwapa watu manyunyu ya mvua, pia mimea ya shambani kwa ajili ya kila mtu. Sanamu huzungumza udanganyifu, waaguzi huona maono ya uongo; husimulia ndoto ambazo si za kweli, wanatoa faraja batili. Kwa hiyo watu wanatangatanga kama kondoo walioteseka kwa kukosa mchungaji. “Hasira yangu inawaka dhidi ya wachungaji, nami nitawaadhibu viongozi; kwa kuwa BWANA wa majeshi atalichunga kundi lake, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kama farasi mwenye kiburi akiwa vitani. Kutoka Yuda litatokea Jiwe la pembeni, kutoka kwake vitatoka vigingi vya hema, kutoka kwake utatoka upinde wa vita, kutoka kwake atatoka kila mtawala. Kwa pamoja watakuwa kama mashujaa wanaokanyaga barabara za matope wakati wa vita. Kwa sababu BWANA yu pamoja nao, watapigana na kuwashinda wapanda farasi. “Nitaiimarisha nyumba ya Yuda na kuiokoa nyumba ya Yusufu. Nitawarejesha kwa sababu nina huruma juu yao. Watakuwa kama watu ambao sijawahi kuwakataa kwa sababu mimi ndimi BWANA Mungu wao, nami nitawajibu. Waefraimu watakuwa kama mashujaa, mioyo yao itafurahi kana kwamba ni kwa divai. Watoto wao wataona na kufurahi, mioyo yao itashangilia katika BWANA. Nitawaashiria na kuwakusanya ndani. Hakika nitawakomboa, nao watakuwa wengi kama walivyokuwa mwanzoni. Ijapokuwa niliwatawanya miongoni mwa mataifa, hata hivyo wakiwa katika nchi za mbali watanikumbuka mimi. Wao na watoto wao watanusurika katika hatari nao watarudi. Nitawarudisha kutoka Misri na kuwakusanya toka Ashuru. Nitawaleta katika nchi ya Gileadi na Lebanoni, na hapo hapatakuwa na nafasi ya kuwatosha. Watapita katika bahari ya mateso; bahari iliyochafuka itatulizwa na vilindi vyote vya Mto Naili vitakauka. Kiburi cha Ashuru kitashushwa, nayo fimbo ya utawala ya Misri itatoweka. Nitawaimarisha katika BWANA, na katika jina lake watatembea,” asema BWANA.

Shirikisha
Soma Zekaria 10