Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wimbo Ulio Bora 8:1-14

Wimbo Ulio Bora 8:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Laiti ungekuwa kaka yangu, ambaye amenyonyeshwa na mama yangu! Hivyo, hata kama ningekutana nawe nje, ningekubusu na hakuna ambaye angenidharau. Ningekuongoza na kukufikisha nyumbani kwa mama mzazi, mahali ambapo ungenifundisha upendo. Ningekupa divai nzuri iliyokolezwa, ningekupa divai yangu ya makomamanga yangu. Mkono wako wa kushoto u chini ya kichwa changu, na mkono wako wa kulia wanikumbatia. Nawasihini, enyi wanawake wa Yerusalemu, msiyachochee wala kuyaamsha mapenzi, hadi hapo wakati wake utakapofika. Ni nani huyu ajaye kutoka mbugani, huku anamwegemea mpenzi wake? Chini ya mtofaa, mimi nilikuamsha, pale ambapo mama yako aliona uchungu, naam, pale ambapo mama yako alikuzaa. Nipige kama mhuri moyoni mwako, naam, kama mhuri mikononi mwako. Maana pendo lina nguvu kama kifo, wivu nao ni mkatili kama kaburi. Mlipuko wake ni kama mlipuko wa moto, huwaka kama mwali wa moto. Maji mengi hayawezi kamwe kulizima, mafuriko hayawezi kulizamisha. Mtu akijaribu kununua pendo, akalitolea mali yake yote, atakachopata ni dharau tupu. Tunaye dada mdogo, ambaye bado hajaota matiti. Je, tumfanyie nini dada yetu siku atakapoposwa? Kama angalikuwa ukuta, tungalimjengea mnara wa fedha; na kama angalikuwa mlango, tungalimhifadhi kwa mbao za mierezi. Mimi nalikuwa ukuta, na matiti yangu kama minara yake. Machoni pake nalikuwa kama mwenye kuleta amani. Solomoni alikuwa ana shamba la mizabibu, mahali paitwapo Baal-hamoni. Alilikodisha kwa walinzi; kila mmoja wao alilipa vipande elfu vya fedha. Shamba langu la mizabibu ni shamba langu mwenyewe, naam, ni shamba langu binafsi! Basi, Solomoni, wewe ukae na elfu zako za fedha, na kila mlinzi wa matunda akae na mia mbili zake. Ewe uliye shambani, rafiki zangu wanasikiliza sauti yako; hebu nami niisikie tafadhali! Njoo haraka ewe mpenzi wangu, kama paa au mwanapaa dume juu ya milima ya manukato.

Wimbo Ulio Bora 8:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Laiti ungekuwa kama ndugu yangu, Aliyeyanyonya matiti ya mamangu! Kama ningekukuta huko nje, Ningekubusu, asinidharau mtu. Ningekuongoza nyumbani mwa mamangu, Naye angenifundisha; Ningekunywesha divai iliyokolea, Divai mpya ya mkomamanga wangu. Mkono wake wa kushoto ungekuwa chini ya kichwa changu, Nao wa kulia ungenikumbatia. Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Msiyachochee mapenzi, au kuyaamsha, Hadi yatakapokuwa tayari. Ni nani huyu apandaye kutoka nyikani, Akimtegemea mpendwa wake? Nilikuamsha chini ya huo mpera; Huko mama yako alikuonea uchungu, Aliona uchungu aliyekuzaa. Nitie kama mhuri moyoni mwako, Kama mhuri juu ya mkono wako; Kwa maana upendo una nguvu kama mauti, Na wivu ni mkali kama ahera. Mwako wake ni mwako wa moto, Na miali yake ni miali ya Yahu. Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, Wala mito haiwezi kuuzamisha; Kama mtu angetoa badala ya upendo Mali yote ya nyumbani mwake, Angedharauliwa kabisa. Kwetu sisi tuna dada mdogo, Wala hana matiti; Tumfanyieje dada yetu, Siku atakapoposwa? Kama akiwa tu ukuta, Tumjengee buruji za fedha; Na kama akiwa ni mlango, Tumhifadhi kwa mbao za mierezi. Mimi nilikuwa ukuta, Na matiti yangu kama minara; Ndipo nikawa machoni pake Kama mtu aliyeipata amani. Sulemani alikuwa na shamba la mizabibu huko Baal-hamomi Akawakodisha walinzi hilo shamba lake la mizabibu; Kila mtu atoe vipande elfu moja vya fedha kwa matunda yake. Shamba langu la mizabibu, lililo langu mimi, liko mbele yangu. Basi, Sulemani, wewe uwe na elfu zako, Na hao wayalindao matunda yake wapewe mia mbili. Wewe ukaaye bustanini, Hao rafiki huisikiliza sauti yako; Unisikizishe mimi. Ukimbie, mpendwa wangu, Nawe uwe kama paa, au ayala, Juu ya milima ya manukato.

Wimbo Ulio Bora 8:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Laiti ungekuwa kama ndugu yangu, Aliyeyanyonya matiti ya mamangu! Kama ningekukuta huko nje, Ningekubusu, asinidharau mtu. Ningekuongoza nyumbani mwa mamangu, Naye angenifundisha; Ningekunywesha divai iliyokolea, Divai mpya ya mkomamanga wangu. Mkono wake wa kushoto ungekuwa chini ya kichwa changu, Nao wa kuume ungenikumbatia. Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwani kuyachochea mapenzi, au kuyaamsha, Hata yatakapoona vema? Ni nani huyu apandaye kutoka nyikani, Akimtegemea mpendwa wake? Nalikuamsha chini ya huo mpera; Huko mama yako alikuonea utungu, Aliona utungu aliyekuzaa. Nitie kama muhuri moyoni mwako, Kama muhuri juu ya mkono wako; Kwa maana upendo una nguvu kama mauti, Na wivu ni mkali kama ahera. Mwako wake ni mwako wa moto, Na miali yake ni miali ya Yahu. Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, Wala mito haiwezi kuuzamisha; Kama mtu angetoa badala ya upendo Mali yote ya nyumbani mwake, Angedharauliwa kabisa. Kwetu sisi tuna umbu mdogo, Wala hana maziwa; Tumfanyieje umbu letu, Siku atakapoposwa? Kama akiwa tu ukuta, Tumjengee buruji za fedha; Na kama akiwa ni mlango, Tumhifadhi kwa mbao za mierezi. Mimi nalikuwa ukuta, Na maziwa yangu kama minara; Ndipo nikawa machoni pake Kama mtu aliyeipata amani. Sulemani alikuwa na shamba la mizabibu huko Baal-hamomi Akawakodisha walinzi hilo shamba lake la mizabibu; Kila mtu atoe vipande elfu vya fedha kwa matunda yake. Shamba langu la mizabibu, lililo langu mimi, li mbele yangu. Basi, Sulemani, wewe uwe na elfu zako, Na hao wayalindao matunda yake wapewe mia mbili. Wewe ukaaye bustanini, Hao rafiki huisikiliza sauti yako; Unisikizishe mimi. Ukimbie, mpendwa wangu, Nawe uwe kama paa, au ayala, Juu ya milima ya manukato.

Wimbo Ulio Bora 8:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Laiti ungekuwa kwangu kama ndugu wa kiume, ambaye aliyanyonya matiti ya mama yangu! Kisha, kama ningekukuta huko nje, ningekubusu, wala hakuna mtu yeyote angenidharau. Ningekuongoza na kukuleta katika nyumba ya mama yangu, yeye ambaye amenifundisha. Ningekupa divai iliyokolezwa unywe, asali ya maua ya mikomamanga yangu. Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, na mkono wake wa kuume unanikumbatia. Binti za Yerusalemu, ninawaagiza: msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe. Ni nani huyu anayekuja kutoka nyikani akimwegemea mpenzi wake? Nilikuamsha chini ya mtofaa, huko mama yako alipotunga mimba yako, huko yeye alipata uchungu akakuzaa. Nitie kama muhuri moyoni mwako, kama muhuri kwenye mkono wako; kwa maana upendo una nguvu kama mauti, wivu wake ni mkatili kama Kuzimu. Unachoma kama mwali wa moto, kama mwali mkubwa wa moto wa BWANA hasa. Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, mito haiwezi kuugharikisha. Kama mtu angetoa mali yote ya nyumbani mwake kwa ajili ya upendo, angedharauliwa kabisa. Tunaye dada mdogo, matiti yake hayajakua bado. Tutafanya nini kwa ajili ya dada yetu wakati atakapokuja kuposwa? Kama yeye ni ukuta, tutajenga minara ya fedha juu yake. Na kama yeye ni mlango, tutamzungushia mbao za mwerezi. Mimi ni ukuta, nayo matiti yangu ni kama minara. Ndivyo ambavyo nimekuwa machoni pake kama yule anayeleta utoshelevu. Sulemani alikuwa na shamba la mizabibu huko Baal-Hamoni; alikodisha shamba lake la mizabibu kwa wapangaji. Kila mmoja angeleta kwa ajili ya matunda yake shekeli elfu moja za fedha. Lakini shamba langu la mizabibu ambalo ni langu mwenyewe ni langu kutoa; hizo shekeli elfu moja ni kwa ajili yako, ee Sulemani, na shekeli mia mbili ni kwa ajili ya wale wanaotunza matunda yake. Wewe ukaaye bustanini pamoja na rafiki mliohudhuria, hebu nisikie sauti yako! Njoo, mpenzi wangu, uwe kama paa au kama ayala mchanga juu ya milima iliyojaa manukato.