Wimbo Ulio Bora 5:2-16
Wimbo Ulio Bora 5:2-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Nililala, lakini moyo wangu haukulala. Sauti ya mpenzi wangu anabisha hodi. “Nifungulie, dada yangu mpenzi wangu, bibiarusi wangu, hua wangu, usiye na kasoro. Kichwa changu kimelowa umande na nywele zangu manyunyu ya usiku.” Nimekwisha yavua mavazi yangu, nitayavaaje tena? Nimekwisha nawa miguu yangu, niichafueje tena? Hapo mpenzi wangu akaugusa mlango, moyo wangu ukajaa furaha. Niliinuka kumfungulia mpenzi wangu. Mikono yangu imejaa manemane, na vidole vyangu vyadondosha manemane, nilipolishika komeo kufungua mlango. Nilimfungulia mlango mpenzi wangu, lakini kumbe, alikuwa amekwisha toweka. Moyo wangu ulifurahi alipokuwa akizungumza! Nilimtafuta, lakini sikumpata; nilimwita, lakini hakuniitikia. Walinzi wa mji waliniona, walipokuwa wanazunguka mjini; wakanipiga na kunijeruhi; nao walinzi wa lango wakaninyanganya shela langu. Nawasihini, enyi wanawake wa Yerusalemu, mkimwona mpenzi wangu, mwelezeni kwamba naugua kwa mapenzi! Ewe upendezaye kuliko wanawake wote! Kwani huyo mpenzi wako ana nini cha zaidi ya mpenzi mwingine, hata utusihi kwa moyo kiasi hicho? Mpenzi wangu ni mzuri na mwenye nguvu, mashuhuri miongoni mwa wanaume elfu kumi. Kichwa chake kizuri kama dhahabu safi, nywele zake ni za ukoka, nyeusi ti kama kunguru. Macho yake ni kama ya hua kandokando ya kijito, ni kama njiwa waliooga maziwa kando ya kijito. Mashavu yake ni kama matuta ya rihani kama bustani iliyojaa manukato na manemane. Midomo yake ni kama yungiyungi, imelowa manemane kwa wingi. Mikono yake imewekwa bangili za dhahabu, amevalia johari za Tarshishi. Kiwiliwili chake ni kama pembe za ndovu zilizopambwa kwa vito vya johari ya rangi ya samawati. Miguu yake ni kama nguzo za alabasta zilizosimikwa katika misingi ya dhahabu. Umbo lake ni kama Lebanoni, ni bora kama miti ya mierezi. Kinywa chake kimejaa maneno matamu, kwa ujumla anapendeza. Basi, hivyo ndivyo alivyo mpenzi wangu, naam, ndivyo alivyo rafiki yangu, enyi wanawake wa Yerusalemu.
Wimbo Ulio Bora 5:2-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nilikuwa nimelala, lakini moyo wangu uko macho, Sikiliza! Mpendwa wangu anabisha! Nifungulie, dada yangu, mpenzi wangu, Hua wangu, mkamilifu wangu, Kwa maana kichwa changu kimelowa umande, Nywele zangu zina manyunyu ya usiku. Nimeivua kanzu yangu; niivaeje? Nimenawa miguu; niichafueje? Mpendwa wangu aliutia mkono wake tunduni, Na moyo wangu ukasisimuka kwa ajili yake. Nikaondoka nimfungulie mpendwa wangu; Mikono yangu ilidondosha manemane, Na vidole vyangu matone ya manemane, Penye vipini vya komeo. Nilimfungulia mpendwa wangu, Lakini mpendwa wangu amegeuka amepita; (Nimezimia nafsi yangu aliponena), Nikamtafuta, nisimpate, Nikamwita, asiniitikie. Walinzi wazungukao mjini waliniona, Wakanipiga na kunitia jeraha, Walinzi walindao kuta zake Wakaninyang'anya shela yangu. Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Ninyi mkimwona mpendwa wangu, Ni nini mtakayomwambia? Ya kwamba nazimia kwa mapenzi. Mpendwa wa namna gani ni mpendwa wako, Wewe uliye mzuri katika wanawake, Mpendwa wa namna gani ni mpendwa wako, Hata wewe utusihi hivyo? Mpendwa wangu ni mweupe, tena mwekundu, Mashuhuri miongoni mwa elfu kumi; Kichwa chake ni kama dhahabu safi sana, Nywele zake ni za ukoka, nyeusi kama kunguru; Macho yake ni kama hua penye vijito, Wakioga kwa maziwa, wakiikalia mito iliyojaa; Mashavu yake ni kama matuta ya rihani Ambayo hufanyizwa manukato; Midomo yake ni kama nyinyoro, Inadondosha matone ya manemane; Mikono yake ni kama mianzi ya dhahabu, lliyopambwa kwa zabarajadi; Kiwiliwili chake kama kazi ya pembe, Iliyonakishiwa kwa yakuti samawi; Miguu yake ni kama nguzo za marimari, Zilizowekwa juu ya misingi ya dhahabu; Sura yake ni kama Lebanoni, Ni bora mfano wa mierezi; Kinywa chake kimejaa maneno matamu, Ndiye mzuri sana kwa ujumla. Ni huyu mpendwa wangu, ni huyu rafiki yangu, Enyi binti za Yerusalemu.
Wimbo Ulio Bora 5:2-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nalikuwa nimelala, lakini moyo wangu u macho, Sikiliza! Mpendwa wangu anabisha! Nifungulie, umbu langu, mpenzi wangu, Hua wangu, mkamilifu wangu, Kwa maana kichwa changu kimelowa umande, Nywele zangu zina manyunyu ya usiku. Nimeivua kanzu yangu; niivaeje? Nimeitawadha miguu; niichafueje? Mpendwa wangu aliutia mkono wake tunduni, Na moyo wangu ukachomeka kwa ajili yake. Nikaondoka nimfungulie mpendwa wangu; Mikono yangu ilidondoza manemane, Na vidole vyangu matone ya manemane, Penye vipini vya komeo. Nalimfungulia mpendwa wangu, Lakini mpendwa wangu amegeuka amepita; (Nimezimia nafsi yangu aliponena), Nikamtafuta, nisimpate, Nikamwita, asiniitikie. Walinzi wazungukao mjini waliniona, Wakanipiga na kunitia jeraha, Walinzi walindao kuta zake Wakaninyang’anya shela yangu. Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Ninyi mkimwona mpendwa wangu, Ni nini mtakayomwambia? Ya kwamba nazimia kwa mapenzi. Mpendwa wa namna gani ni mpendwa wako, Wewe uliye mzuri katika wanawake, Mpendwa wa namna gani ni mpendwa wako, Hata wewe utusihi hivyo? Mpendwa wangu ni mweupe, tena mwekundu, Mashuhuri miongoni mwa elfu kumi; Kichwa chake ni kama dhahabu safi sana, Nywele zake ni za ukoka, nyeusi kama kunguru; Macho yake ni kama hua penye vijito, Wakioga kwa maziwa, wakiikalia mito iliyojaa; Mashavu yake ni kama matuta ya rihani, Ambayo hufanyizwa manukato; Midomo yake ni kama nyinyoro, Inadondoza matone ya manemane; Mikono yake ni kama mianzi ya dhahabu, lliyopambwa kwa zabarajadi; Kiwiliwili chake kama kazi ya pembe, Iliyonakishiwa kwa yakuti samawi; Miguu yake ni kama nguzo za marimari, Zilizowekwa juu ya misingi ya dhahabu; Sura yake ni kama Lebanoni, Ni bora mfano wa mierezi; Kinywa chake kimejaa maneno matamu, Ndiye mzuri sana pia pia. Ni huyu mpendwa wangu, ni huyu rafiki yangu, Enyi binti za Yerusalemu.
Wimbo Ulio Bora 5:2-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nililala lakini moyo wangu ulikuwa macho. Sikiliza! Mpenzi wangu anabisha: “Nifungulie, dada yangu, mpendwa wangu, hua wangu, usiye na hitilafu. Kichwa changu kimeloa umande, na nywele zangu manyunyu ya usiku.” Nimevua joho langu: je, ni lazima nivae tena? Nimenawa miguu yangu: je, ni lazima niichafue tena? Mpenzi wangu aliweka mkono wake kwenye tundu la komeo; moyo wangu ulianza kugonga kwa ajili yake. Niliinuka kumfungulia mpenzi wangu, mikono yangu ikidondosha manemane, vidole vyangu vikitiririka manemane, penye vipini vya komeo. Nilimfungulia mpenzi wangu, lakini mpenzi wangu alishaondoka; alikuwa ameenda zake. Moyo wangu ulishuka kwa kuondoka kwake. Nilimtafuta lakini sikumpata. Nilimwita lakini hakunijibu. Walinzi walinikuta walipokuwa wakifanya zamu za ulinzi mjini. Walinipiga, wakanijeruhi, wakaninyangʼanya joho langu, hao walinzi wa kuta! Enyi binti za Yerusalemu, ninawaagiza: mkimpata mpenzi wangu, mtamwambia nini? Mwambieni ninazimia kwa mapenzi. Je, mpenzi wako ni bora kuliko wengine namna gani, wewe uliye mzuri kupita wanawake wote? Je, mpenzi wako ni mzuri kuliko wengine, namna gani, hata unatuagiza hivyo? Mpenzi wangu anangʼaa, tena ni mwekundu, wa kuvutia miongoni mwa wanaume kumi elfu. Kichwa chake ni dhahabu safi kuliko zote, nywele zake ni za mawimbi na ni nyeusi kama kunguru. Macho yake ni kama ya hua kandokando ya vijito vya maji, aliyeogeshwa kwenye maziwa, yaliyopangwa kama vito vya thamani. Mashavu yake ni kama matuta ya mimea ya manukato. Midomo yake ni kama yungiyungi inayodondosha manemane. Mikono yake ni fimbo za dhahabu iliyopambwa kwa krisolitho. Mwili wake ni kama pembe ya ndovu iliyongʼarishwa iliyopambwa na yakuti samawi. Miguu yake ni nguzo za marumaru zilizosimikwa katika vitako vya dhahabu safi. Sura yake ni kama Lebanoni, bora kama miti yake ya mierezi. Kinywa chake chenyewe ni utamu, kwa ujumla yeye ni wa kupendeza. Huyu ndiye mpenzi wangu, huyu ndiye rafiki yangu, ee binti za Yerusalemu.